"Ni matusi" Akothee alalamika kuwekwa kwenye orodha ya wanamuziki matajiri Afrika Mashariki

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa amejikita katika kusimamia utajiri wake mkubwa.

Muhtasari

•Akothee alidai kuondolewa kwenye orodha hiyo akibainisha kuwa tayari amepita hatua ya kuorodheshwa miongoni mwa wanamuziki tajiri zaidi.

•Alibainisha kuwa ni tusi kumuorodhesha miongoni mwa wanamuziki tajiri na akadai kuwekwa kwenye orodha ya wenye mali nyingi zaid

Esther Akoth
Image: HISANI

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee ameibua malalamishi baada ya kujumuishwa katika orodha ya jarida la Forbes ya wanamuziki matajiri zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika taarifa yake ya siku ya Jumatano, mama huyo wa watoto watano alidai kuondolewa kwenye orodha hiyo akibainisha kuwa tayari amepita hatua ya kuorodheshwa miongoni mwa wanamuziki tajiri zaidi.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 aliendelea kueleza kuwa kwa sasa amejikita katika kusimamia utajiri wake mkubwa.

"Sasa nani ameniweka kwa hii orodha? Mnitoe kwa hii orodha kabisa, mimi katika orodha ya matajiri nilipita kitambo kaka, nasimamia utajiri wangu.Sipendi madharau ndogo ndogo," alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Alibainisha kuwa ni tusi kumuorodhesha miongoni mwa wanamuziki tajiri na akadai kuwekwa kwenye orodha ya wenye mali nyingi zaidi.

"Jua tofauti kati ya 1. kusawazisha bili na kusimamia mali. Ninahisi kama kuanzisha matatizo," alisema.

Hivi majuzi, jarida maarufu la Forbes lilichapisha orodha ya wanamuziki matajiri zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuwajumuisha baadhi ya vigogo wa muziki wa Kenya, Tanzania na Uganda.

Orodha hiyo ilitawaliwa pakubwa na wanamuziki wa kiume, Akothee akiwa wa kike pekee katika kumi bora.

Kulingana na Forbes, mwimbaji wa Uganda aliyegeuka kuwa mwanasiasa, Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine ndiye msanii tajiri kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki akiwa na utajiri wa dola za Kimarekani milioni 9.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na staa wa Bongo Diamond  Platnumz ambaye utajiri wake kutoka kwa biashara zake za vyombo vya habari, lebo na kampuni ya ubashiri vyote vinajumuisha dola za Kimarekani milioni 8.2.

Mkongwe wa muziki, Jose Chameleone aliorodheshwa katika nafasi ya tatu akifuatiwa na Akothee wa Kenya, Professor Jay, Alikiba wote wa Tanzania kisha akafuata mwanasiasa wa Kenya Charles Njagua almaarufu Jaguar 

Bosi wa Konde Music Worldwide, Harmonize alitajwa katika nafasi ya nane akifuatiwa na bendi ya muda mrefu kutoka Kenya, Sauti Sol na mwanamuziki mkongwe wa Uganda, Bebe Cool akafunga kumi bora.