Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize kwa mara nyingine ameonyesha upendo na sapoti kubwa kwa mwimbaji mwenzake Rayvanny.
Siku ya Ijumaa, Harmonize alimsifia bosi huyo wa Next Level Music huku akimtambua kama ndugu yake na mwimbaji wake pendwa.
"Mwimbaji wangu pendwa na kaka chui," Konde Boy alisema chini ya chapisho moja la Rayvanny kwenye mtandao wa Instagram.
Rayvanny alimjibu, "Barikiwa sana Konde Bway."
Harmonize alikuwa ametoa maoni kwenye chapisho la mwenzake huyo wa zamani katika lebo ya WCB ambapo aliwaomba mashabiki wake kuchagua wimbo wanaoupenda zaidi katika albamu yake mpya ya 'Flowers III.'
"Chagua wimbo wako bora Mapema!!! Wako namba ngapi #FlowersIII," Msanii huyo wa zamani wa WCB aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuambatanisha na bango la nyimbo tisa zilizo kwenye albamu hiyo.
Rayvanny na Harmonize walizika tofauti zao mapema mwaka huu, miezi michache tu baada ya bosi huyo wa NLM kugura WCB.
Mwezi Februari, wasanii hao wawili ambao waliwahi kuwa chini ya usimamizi wa WCB walianza kufuatiliana tena kwenye Instagram baada ya kuwa wamezuiana kwenye mtandao huo wa kijamii kwa muda mrefu.
Hatua hiyo ilijiri wiki chache tu baada ya wawili hao kutupiana cheche za maneno kwenye mitandao ya kijamii. Vita vya maneno baina yao vilianza baada ya Harmonize kuwashauri wasanii dhidi ya nyimbo za pombe.
Mzozo kati ya mastaa hao wawili ulitimbuka mwaka 2021 baada ya Rayvanny kudaiwa kuanika picha za uchi za Harmonize. Wakati huo, Harmonize alikuwa akichumbiana na muigizaji wa filamu Bongo, Frida Kajala Masanja huku Rayvanny akitoka kimapenzi na binti yake wa pekee, Paula Paul.
Wakati vita vyao vya mtandaoni vikiendelea mapema mwaka huu, Konde Boy alimuuliza msanii huyo mwenzake kwa nini anamchukia sana. Bosi huyo wa Kondegang pia alichukua fursa hiyo kumkumbusha kuhusu mzozo wao wa hapo awali ambao ulivunja mahusiano yake na Kajala mwaka wa 2021.
"Ulifanya kila mtu aone sehemu yangu ya siri, ulitaka nijiuwe na bado niko hapa. Usinichukie wenda Mungu ananiweka kwaajili yako uendelee kuwa inspired . Kuja kwa nyumba yangu nitakuonyesha jinsi ya kutengeneza pesa uweze kulipa label (WCB) ili uweze kutoka kabisa," Aliandika Harmonize.
Harmonize na Rayvanny waliwahi kuwa pamoja katika lebo ya WCB ambayo inasimamiwa na Diamond Platnumz. Wawili hao hata hivyo tayari wamegura lebo hiyo na kuanzisha lebo zao kivyao.