Harmonize kufungua lebo yake ni kama mwendelezo wa Wasafi, namkubali - Diamond

"Kwa sababu nina mchango kwa kiasi kikubwa katika maisha ya muziki wa Harmonize, hata anifanyie ubaya kiasi gani, hawezi kupitiliza ubaya kama mtu hajawahi kunijua" - Diamond.

Muhtasari

• Msanii huyo alifunguka kuwa hivi karibuni atawatangaza wasanii wengine wapya kwenye lebo ya Wasafi.

• Kuondoka kwao na kwenda kuanzisha lebo, kuanzisha nini ni kama mwendelezo tu wa Wasafi na hilo hunipa motisha sana,” Simba alitema.

Harmonzie, Diamond Platnumz
Harmonzie, Diamond Platnumz
Image: Instagram

Kwa mara ya kwanza kabisa, msanii kutoka WCB Wasafi ambaye pia ni mkurugenzi wa lebo hiyo Diamond Platnumz amezungumza kwa mapana na marefu ni jinsi gani anajihisi kumuona aliyekuwa msanii wake Harmonize anavyozidi kutanua mbawa kimuziki n ahata kumpa changamoto katika tasnia ya Bongo Fleva.

Msanii huyo alikuwa anazungumza katika kipindi cha moja kwa moja mtandaoni na jamaa mmoja ambaye alimtupia swali hilo kutaka kujua Simba anajihisije na kama kweli kuna uhasama wa kimuziki baina yake na Harmonize.

Diamond alisema kuwa Harmonize amempa faraja kubwa sana ya kupitia mikononi mwake na kwenda kule nje kuweza kujisimamia – ni jambo ambalo linampa furaha kubwa sana kama baba yeyote anapomlea mtoto na kuja kumuona akifanya vyema katika kitu ambacho alimfunza na kumkuza nacho.

“Kwanza ni faraja kubwa kwangu, mimi ujue nimepata bahati, nina bahati kubwa ukizingatia kwamba wasanii wangu wote wanafanya vizuri sana kimuziki. Wasanii wote ambao wamepitia mikononi mwangu Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Zuchu na wengine wanafanya vizuri mno. Na kusema kweli hilo linanipa msukumo wa faraja nahisi kwamba hawajanifeli kama mzazi,” msanii huyo alisema.

Diamond alifichua sababu yake kupakia chati za muziki ambazo zinaonesha majina na takwimu za wasanii wote kwenye majukwaa ya kidijitali ya kupakua muziki, akisema kuwa raha yake hutokana na pale anapowaona wote waliopitia mikononi mwake wakijaribu kumpa changamoto kwenye takwimu hizo.

“Nasikia raha nikiona kama wasanii ambao wametoka kwenye mikono yangu ndio wako kwenye zile takwimu. Sio kwa ubaya lakini kwa sababu ni raha. Mimi muda Fulani huwa tu naandika namba 1,2,3…6..n.k ni kitu kizuri sana. Kuondoka kwao na kwenda kuanzisha lebo, kuanzisha nini ni kama mwendelezo tu wa Wasafi na hilo hunipa motisha sana,” Simba alitema ukweli wake.

Diamond alisema kuwa kufanya vizuri kwa wasanii ambao amewakuza kunampa msukumo Zaidi na kufichua hivi karibuni atawasaini wasanii wengine wawili wapya kwenye lebo ya Wasafi.

“Hili hunipa motisha sana kuendelea kuwatoa wasanii wengi wapya. Kama nilivyosema ninatarajia kutoa wasanii wengine wawili. Unajua mtu kwa njia moja au nyingine una mchango katika jambo analolifanya, hawezi kukufanyia mabaya yakupitiliza kama yule ambaye hajawahi kukujua,” Diamond alisema alimlenga Harmonize.