Mchungaji maarufu kutoka taifa jirani la Tanzania Daniel Mgogo amefichua na kufafanua siri iliyopo nyuma ya maisha marefu ya wanawake ikilinganishwa na wanaume.
Kulingana na Mchungaji Mgogo, wanawake wanaishi miaka mingi duniani kwa sababu wao aghalabu huongea na kuongea ni njia moja ya kuondoa msongo wa mawazo.
Mgogo alisema kuwa kiuhalisia, wanawake ni viumbe wa kelele ikilinganishwa na wanaume ambao wameumbwa kuwa kimya kimya na mambo yao pasi na kumwambia mtu.
“Kiujumla wakati mwingine wanawake hawajui falsafa na saikolojia ya kukaa na mwanamume. Mwanamume ni kiumbe Fulani ambacho hakitaki kelele. Lakini wakati huo huo pia, mwanamke ni kiumbe cha kelele. Ndio maana wanasema wanawake wanaishi miaka mingi kwa sababu wanatoa msongo wa mawazo,” mchungaji Mgogo alisema.
Mgogo alitumia fursa hiyo kufafanua kwa kutoa ushauri kwa wanaume walioona kuwaruhusu wake zao kupiga kelele kwani ndivyo walivyoumbwa.
“Mruhusu mke wako apige kelele, yaani aongee kwa sababu wao hiyo ndio njia ya kutoa sumu miilini. Wao wanakaa miaka mingi duniani kwa sababu wanatoa ‘stress’ lakini sisi huwa hatusemi sana kwa hiyo huwa hatutoi sumu miilini, tunakaa bila kuitoa na tunakufa haraka,” Mgogo alihoji.
Mchungaji Mgogo pia aliwashauri wanawake kuwakaribia wanaume zao kwa ustaarabu kwani si watu wanaopenda kelele.
“Mwanaume hata kama amekosea anataka aonywe kwa ustaarabu. Huwa hataki kelele, mwelekeze kwa upole kwamba bwana hili liko hivi, lakini ukifika kwake unahema moto ni kama unamghasi hasira zake,” mchungaji alishauri.
“Hata kama kuna makosa mahali Fulani, mpikie chai, mpikie chakula wakati ametulia ndio unamuuliza.”