Davido na mkewe Chioma wamvulia kofia Harmonize, wakiri kupenda kazi yake

Staa huyo wa Afrobeats amekiri kuupenda sana wimbo maarufu wa Harmonize, 'Single Again'.

Muhtasari

•Huku akimshukuru mwimbaji huyo wa Nigeria, Konde Boy alimtakia yeye na familia yake baraka tele maishani.

•Harmonize alimtambua mtunzi huyo wa kibao 'Unavailable' kama G.0.AT. yaani, mwimbaji bora zaidi wa muda wote.

katika picha ya maktaba
Harmonize na Davido katika picha ya maktaba
Image: HISANI

Mwimbaji  wa Afrobeats, David Adedeji Adeleke almaarufu Davido amekiri kuupenda sana wimbo maarufu wa  Harmonize,  'Single Again'.

Siku ya Jumamosi, staa huyo wa Bongo alitoa shukrani kwa Davido baada ya kumtumia ujumbe kwenye Instagram akimfichulia jinsi yeye na mkewe Chioma Rowland wanavyoushabikia wimbo huo ambao aliachia mwezi Februari.

"Mimi na mke wangu tunaupenda wimbo huu," Davido alimwandikia na kuambatanisha na picha ya wimbo huo kwenye YouTube.

Huku akimshukuru mwimbaji huyo wa Nigeria, Konde Boy alimtakia yeye na familia yake baraka tele maishani.

"Mungu abariki familia hii nzuri," alimwambia.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide aliendelea kumtambua mtunzi huyo wa kibao 'Unavailable' kama G.0.AT. yaani, mwimbaji bora zaidi wa muda wote.

Harmonize kwa sasa yuko nchini Marekani ambako ameandaa shoo  kadhaa kabla ya kuelekea Uingereza na Australia. Pia ametangaza tamasha zaidi zitakazofanyika baadaye katika mataifa mbalimbali ya Afrika na Ulaya.

Siku ya Jumamosi jioni alipiga shoo jijini Indianapolis, Marekani ambapo kundi la mashabiki wake walijitokeza kutumbuizwa.

Ziara ya staa huyo wa Bongo ya Marekani inakuja wiki chache tu baada ya Davido kutangaza ziara ya kimuziki nchini humo. Mwimbaji huyo wa Nigeria atatumbuiza katika maeneo mbalimbali ya America mwezi Julai.

Wiki chache zilizopita, Davido alikosolewa baada ya kudaiwa kumpa mimba mzazi mwenzake anayeishi katika nchi hiyo ya Magharibi.

Kulingana na ripoti, Amanda ambaye ana mtoto mwingine na mwanamuziki huyo anaishi katika jimbo la Atlanta, Marekani ambako Davido amekuwa akitembea mara kwa mara katika ziara zake za Marekani.

Muda wa kuzaliwa kwa mtoto huyo ndio umewafanya wanamitandao kuonesha hasira. Inadaiwa ilitokea alipokuwa akifunga ndoa na Chioma wakati wote walikuwa na majonzi ya kifo cha mtoto wao.

Kuna madai zaidi kwamba Davido alijaribu kumpa mwanamke huyo shinikizo la kutoa mimba hiyo.

Kulingana na mdau wa ndani, Davido alisafiri kwa ndege hadi Amerika katika miezi ya mwanzoni mwa mwaka jana ili kutumia wakati mwingi na Amanda na binti yake wakati yeye na Chioma walikuwa wameachana.

Walakini, baada ya kifo cha Ifeanyi, familia ya Chioma ilisisitiza amuoe ili kuweza kumzika mwana wao.

Siku chache zilizopita, wanandoa hao hata hivyo walitupilia mbali tetesi za kuachana na kuhakikishiana upendo.