"Nilikuwa maarufu kumliko na sivutiwi na pesa zake" - Ex wa Hakimi awajibu wakosoaji

Hiba Abouk alisema walipoanza kuchumbiana 2018, alikuwa maarufu na mwenye pesa kumliko Hakimi na wala kutaka talaka hakuwa na maana ya kutaka utajiri wake.

Muhtasari

• Abouk alisema kwamba kutaka talaka hakukuwa na kusudi lolote la kutaka mgao katika mali ya mchezaji huo.

• Talaka yake ilichochewa na uvumi kwamba Hakimi alimbaka mwanamke kwenye kitanda cha ndoa wakati mkewe na watoto wamenda ziara Dubai.

Mke wa Hakimi amevunja ukimya kufuatia sakata la talaka na kukosa mali.
Mke wa Hakimi amevunja ukimya kufuatia sakata la talaka na kukosa mali.
Image: Twitter

Hiba Abouk, mke wa zamani wa mwanasoka wa Morocco Achraf Hakimi, amekuwa akichukua vichwa vya habari hivi karibuni.

Mwigizaji na mwanamitindo huyo sasa ameibua mapya baada ya kudai kuwa alikuwa maarufu zaidi kuliko mwanasoka huyo walipoanza kuchumbiana mwaka wa 2018.

Hata hivyo, madai haya yamezua utata mwingi, hasa kwa vile alidaiwa kutaka nusu ya utajiri wake baada ya talaka yao.

Abouk amesema kuwa hana nia ya utajiri wa mchezaji huyo, lakini inaonekana watu wengi hawajashawishika na hilo.

Kulingana na ripoti, mwigizaji huyo anadaiwa aligundua kuwa Hakimi alikuwa amesajili mali yake yote kwa jina la mamake. Hii imechochea mjadala kuhusu kama Abouk ana haki ya kupata mgao wa nyota huyo wa PSG.

Licha ya upinzani huo, Abouk anasalia imara katika msimamo wake. Katika mahojiano na mwanahabari Maria Patino kupitia AS, mwigizaji huyo alinyoosha maelezo baada ya kutupiwa swali hilo akisema;

"Habari, María. Ni ulimwengu uliojaa chuki za wanawake tunamoishi. Kwa kuzingatia kwamba, tulipoanzisha uhusiano, hakupata pesa na mimi nilijulikana zaidi kuliko yeye.”

Maoni ya Abouk yamezua mijadala mingi kwenye mitandao ya kijamii, huku watu wengi wakitoa maoni yao kuhusu suala hilo. Baadhi wamemkosoa kwa kudai sehemu ya mali ya Hakimi, huku wengine wakiunga mkono madai yake kwamba alikuwa maarufu kuliko yeye walipoanza kuchumbiana.

Baada ya kutoa tamko hilo, aliyekuwa mumewe Hakimi Jumapili alipakia picha ya pamoja wakiwa na mamake na kumwandikia ujumbe wa kumsherehekea siku ya kina mama, akimtaja kama mhimili muhimu katika maisha yake.

Inabakia kuonekana jinsi hali hii itakavyokuwa, lakini jambo moja ni la uhakika: utata unaozunguka talaka ya Hakimi na Abouk hautaisha hivi karibuni.