Msanii maarufu wa Afrobeats kutoka Nigeria Davido amefichua kwamba atatoa simulizi la maisha yake kupitia jukwaa kubwa Zaidi ya usambazaji wa filamu, Netflix.
Katika mazungumzo ya hivi majuzi na Esquire Middle East, jumba la wanahabari lenye makao yake Dubai, mwimbaji huyo alisema kipindi hicho kitaitwa ‘David’ na kitasimulia maisha yake.
Aliongeza kuwa ni mradi mkubwa na utatoka Desemba.
"Nina filamu inayotoka Desemba na Netflix. Ni kubwa sana,” alisema.
"Hii ni mara ya kwanza kusema chochote kuhusu hilo, kwa kweli. Ni makala-mfululizo wa hati kuhusu maisha yangu unaoitwa 'David'. Sipaswi kuzungumza juu ya hili."
Mnamo Mei 8, Davido aliadhimisha mwaka wake wa 12 katika tasnia ya muziki.
Ikumbukwe mwezi Februari msanii huyo kupitia Instastory yake aliweka kionjo cha simulizi ya msanii kutoka Marekani Kanye West ambayo ilipeperushwa Netflix na Davido aliweka wazi kuvutiwa kwake na hilo.
Inaaminika kuwa huenda hilo lilimpa msukumo wa aina yake mpaka naye kutaka kufanya simulizi kama hilo ambalo amefichua litatoka mwezi Desemba mwaka huu.
Kwa mfululizo wa tuzo na kutajwa kwa heshima, mwimbaji huyo amejidhihirisha kuwa mmoja wa watu wanaoongoza katika tasnia ya muziki barani Afrika.
Alitoa 'Timeless', albamu yake ya nne iliyohifadhi nyimbo 17, mnamo Machi 31.
Tangu kutolewa kwa albamu hiyo, ‘Timeless’ imeendelea kukusanya mamilioni ya mitiririko katika majukwaa ya muziki.
Mnamo Aprili 10, ilipata nafasi ya 37 kwenye chati ya Billboard 200 ya Marekani.
Albamu hiyo pia iliweka rekodi yake ya siku ya kwanza ya utiririshaji wa albamu ya Kiafrika kwenye Apple Music katika mwezi huo huo.