Nilihubiri redioni kwa miaka 4 bila malipo - Lofty Matambo

Wafuasi wake walikuwa wanasema kuwa analipwa vinono ila Lofty anadhihirisha kuwa alijitolea kufanya bila malipo.

Muhtasari

• Matambo alifunguka na kusema kuwa alifanya kwa miaka zaidi ya minne bila malipo.


Image: Lofty Matambo

Loft Matambo ambaye ni mwanahabari na mhariri wa kitengo cha Kiswahili kwenye runinga ya NTV, anasema kwamba alianya kazi ya kuhubiri redioni kwa miaka minne bila malipo.

Katika mahojiano baina yake na mwanablogu Makena siku ya sherehe ya kuwasherehekea walioshinda kategoria kadhaa za uanahabari wa mwaka Matambp alifunguka kuwa alikuwa anafanya hivyo si kwa kushurutishwa bali ni kwa kujitolea tu.

"Nilikuwa naamka alfajiri saa kumi kuenda kuhubiri katika redio mojawapo na kwa kipindi kirefu watu wasichokijua kwamba najitolea walikuwa wananiona kwenye runinga usiku, wananiona kwenye redio alfajiri, wanasema kuwa nalipwa vinono na naitwa kama mgeni mheshimiwa kwa kuwa wanaona nafanya kazi nyingi kwenye redio na runinga."

Matambo anasema kuwa aliacha kazi ambayo ni mkataba na ya kudumu akachukua ajira ya uanahabari, kandarasi ya miezi sita na alijitolea kufanya kazi kwa miaka zaidi ya minne bila malipo ili aweze kukua.

"Nimehama kutoka mji mmoja hadi mji mwingine na nimeishi mpaka Garissa kwa sababu natafuta ndoto yangu," Matambo alisema.

Isitoshe mhariri huyo anadai kuwa, baadhi ya vitu ambavyo anaangalia nyuma anasema kweli jitihada hulipa.

"Sasa hivi navaa Kiswahili changu, uanahabari wangu, buti langu ni uanahabari wangu, mkanda wangu pia ni uanahabari wangu kwa hivyo nashukuru," alisema mwanahabari huyo.