Wanablogu wanatengeneza pesa nyingi kutoka video za kunihoji, lakini mbona hawanipi kitu?

Yesu wa Tongaren alionesha kutofurahishwa kwake akisema kuwa wanahabari ni wagumu kurudisha shukrani ya hata angalau shilingi elfu moja tu.

Muhtasari

• Alifichua kuwa watu wengi wamemfahamisha kwamba wanahabari wamepata faida kubwa kutokana na mazungumzo yao naye.

• "Lakini naskia tu watu wakisema kwa nini hawakupatii kitu,” Yesu wa Tongaren alisema.

Yesu wa Tongaren
Image: HISANI

Mhubiri mwenye utata kutoka Bungoma Eliud Wekesa, almaarufu Yesu wa Tongaren, amezua mjadala baada ya kutoa ombi kwa wanahabari waonyeshe shukrani zao kwake kwa kutoa sadaka kabla ya kumfanyia mahojiano.

Eliud Wekesa, kama anavyojulikana kwa jina halisi alikuwa akizungumza na wanahabari baada ya kuitikia wito wa kamanda wa polisi kaunti ya Bungoma Francis Kooli aliyemtaka kufika huku kwa mahojiano kuhusu dhehebu lake lenye utata katika jamii.

“Wanahabari, sitahofia kuongea hili na nitasema ukweli, Hta shilingi tu elfu moja kumpe Yesu ni ngumu sana. Lakini naskia tu watu wakisema kwa nini hawakupatii kitu,” Yesu wa Tongaren alisema.

Alifichua kuwa watu wengi wamemfahamisha kwamba wanahabari wamepata faida kubwa kutokana na mazungumzo yao naye.

Walakini, licha ya faida hii ya kifedha, alionyesha kusikitishwa na ukosefu wa urejeshaji, hata kwa njia ya sadaka rahisi, wakati waandishi wa habari wanapomtembelea nyumbani kwake.

Akihutubia wanahabari moja kwa moja, Yesu wa Tongaren alisisitiza umuhimu wa kutambuliwa lakini pia akaashiria kwamba hatua yake ya kuitisha kitu kutoka kwa wanahabari si kuonesha ulafi au kupenda mali ya kidunia bali ni kutaka utambulisho na urejeshi wa shukrani tu.

Hii mambo iko. Lakini huwa siangalii hayo maana hii kazi haikuja tu kwa njia rahisi,” alisema.

Mhubiri huyo mwenye utata alisema kuwa baadhi walikuwa wanamuita maskini, wengine wakisema haonekani kuwa razini, jambo ambalo hata hivyo alilikubali shingo upande akionesha kutofurahishwa nalo.