"Umejisahau ukaanza kushindana na wanawake!" Akothee amjibu Jaguar

Akothee alitema moto huu kwa mbunge huyo wa zamani baada ya kudai kwamba Akothe hawezi kumshinda katika utajiri kama ambavyo Forbes walikuwa wamechapisha.

Muhtasari

• "Tangu lini wanaume wakajisahau na kuanza kushindana na kujilinganisha na WANAWAKE?” Akothee aliuliza.

Akothee amjibu Jaguar kuhusu utajiri wa Forbes
Akothee amjibu Jaguar kuhusu utajiri wa Forbes
Image: Instagram

Siku mbili tu baada ya aliyekuwa mbunge wa Starehe Charles Njagua almaarufu Jaguar kutoa kauli ya kupinga chapisho la Forbes kuhusu wasanii wenye utajiri mkubwa mwaka 2023 Afrika Mashariki, Akothee amemjibu.

Mapema mwaka huu Radio Jambo tuliripoti kwamba Forbes waliorodhesha wasanii wa Afrika Mashariki na utajiri wao na kwenye orodha hiyo ya kumi bora, Akothee ndiye alikuwa msanii wa kike pekee aliyeshikilia nafasi ya nne kwa utajiri wa shilingi bilioni moja, akiwa namba moja kwa wasanii kutoka Kenya.

Jaguar alikuwa namba saba na wa pili nchini Kenya kwa utajiri wa shilingi milioni 927 lakini katika mkutano na wanahabari kutangaza ujio wake upya kwenye muziki, Jaguar alisema kuwa haamini kabisa kuwa Akothee angeweza kumshinda katika utajiri.

“Kama Akothee na Harmonize wamenishinda naeza nikaacha muziki leo!” Jaguar aliwaambia wanahabari hao.

Akothee kwa kumjibu alimtemea mameno makali ya kashfa akisema kuwa mbunge huyo wa zamani ni kama amejichanganya akili na kujisahau mpaka amefikia hatua ya kushindana na wanawake.

“Ati nani amesema yeye ni tajiri kushinda madam Boss? Tangu lini wanaume wakajisahau na kuanza kushindana na kujilinganisha na WANAWAKE?” Akothee aliuliza.

Msanii huyo alizidisha kisu chenye makali kwenye utumbo wa Jaguar akisema kuwa hana kigezo chochote cha kumweka bungeni na kumsuta vikali kuwa aliingia kwenye siasa ili kubaki na ushawishi baada ya kuupoteza katika muziki.

“Kwani una sifa gani za kupata ubunge, kama mtihani ungefanywa kwenye nyadhifa wanazoshikilia baadhi ya wanasiasa 🤣🤣🤣🤣haki wengi wangerudi nyumbani mapema jana jioni 🤣🤣🤣, kwa hiyo kaa mpole mwanasiasa yeyote anayejigamba na pesa za walipa kodi ati "Utajiri" Utajiri kitu Gani,” Akothee alisema.

Akothee alimwambia Jaguar kuwa alikuwa amepoteza ushawishi na alisubiri hadi tukio la Mustafa litokee ili kujitokeza na kupata kuzungumziwa.

“Kila wakati unangojea kitu kinachovuma ili kutumaini ili Uweze kugonga vichwa vya habari kwa sababu siku zingine huna umuhimu.”