Kwa Zaidi ya siku nne sasa, wasanii Jaguar na Akothee wamekuwa wakishambuliana mitandaoni baada ya Jaguar kujitokeza wazi akipuuzilia mbali orodha ya jarida la Forbes kuhusu wasanii wa Afrika Mashariki wenye utajiri mkubwa.
Forbes baada ya kutoa orodha hiyo na kuonesha kuwa Akothee ndiye msanii tajiri Zaidi nchini Kenya kwa kima cha bilioni moja, Jaguar alipinga vikali akisema hawezi kuwa nyuma ya Akothe.
Jaguar alikuwa amesema kuwa ikiwa Akothee anamshinda Utajiri basi yuko radhi kuacha muziki, jambo ambalo halikumfurahisha msanii huyo wa kike aliyemshukia vikali.
Akothee alimdhihaki Jaguar akisema kuwa ameanza kujilinganisha na kujishindanisha na wanawake huku pia akimsuta kuwa hana elimu yoyote na bungeni alikwenda kujificha tu.
Jaguar akijibu mipigo hiyo, amemkomesha Akothee akitumia maneno yaliyonukuliwa kutoka kwa mchungaji mwenye utata Paul Mackenzie akiwaambia watu wanaopingana na dhehebu lake kuwa ‘kitawaramba’.
“Unachokipigania hukijui, kitakuramba Akothee,” Jaguar alisema huku akiwasihi mashabiki wake waendelee kutazama wimbo wake mpya aliomshirikisha Lavalava.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wake walimkebehi kwa kumjibu Akothee, wakisema kuwa angekuwa na heshima za mwanaume kamili iwapo hangechagua vita vya majibizano ya maneno mitandaoni.
“Pigana na wanaume wenzako, unakaa bwege,” Wafula Melvin alimwambia.
“Ukibishana na mwanamke lazima udharaurike ata uwe nani. Ni bora ukae kimya, wanaume hawaongeagi sana. Nakukubali ila hapa umezingua,” Allan Josh alimwambia.