Lupita asimulia maana ya michoro ya hina kwenye kichwa wiki baada ya kunyoa upara

Mwigizaji huyo alisema alikuwa amealikwa kwa harusi na alihangaika kupata muonekano wa kipekee mara ghafla taswira hiyo ikamjia na ikabidi ameifanikisha.

Muhtasari

• Ubunifu huo tata, ulioshirikiwa kwenye Instagram ya Nyong’o, umeenea mtandaoni, na kuvutia mamilioni ya watu ulimwenguni kote.

Lupita Nyong'o azungumzia chimbuko la hina kwenye kichwa chake.
Lupita Nyong'o azungumzia chimbuko la hina kwenye kichwa chake.
Image: Instagram

Mwigizaji kutoka Mexico mwenye asili ya Kenya, Lupita Nyong’o alikuwa gumzo la mitandaoni baada ya kuhudhuria hafla moja ya harusi baada ya kuonekana akiwa na michoro kama tattoo kwenye kichwa chake chote, wiki moja tu baada ya kuonesha mtindo wake mpya wa unyoaji ambao ni upara.

Ubunifu huo tata, ulioshirikiwa kwenye Instagram ya Nyong’o, umeenea mtandaoni, na kuvutia mamilioni ya watu ulimwenguni kote.

Akiwa anajulikana kwa mtindo wake wa kipekee na chaguo la kutokea kijasiri, Nyong’o alifichua kisa cha sura yake ya kugeuza kichwa katika chapisho hilo alilolipa mada, Hadithi ya Kichwa changu.

Alisema kuwa mwaka jana alikutana na mmoja wa marafiki zake katika hafla ya harusi nchini Pakistan na alikuwa amechora michoro hiyo, kitu ambacho kilimfurahisha sana na kujiambia siku moja naye angependa kujichora vile.

“Kulikuwa na kitu cha kipekee kuhusu jinsi alivyojieleza katika sanaa ya hina. Na nilijiahidi, "Siku moja nitakuwa na sababu ya kufanya kazi na Sabeen." Lupita alisema.

Kwa mwaliko wa kuhudhuria usiku wa ufunguzi wa Harusi ya Monsoon, Nyong’o alijipata akihangaika kutafuta vazi lifaalo.

Kuazima sari na vito kutoka kwa rafiki, bado alihisi muonekano haujakamilika. Kisha taswira ya muundo wa hina iliyofunika kichwa chake chenye upara ikamjia akilini na kusema labda ndio ulikuwa wakati mzuri wa kujaribu.

“Na kisha, katikati ya usiku, picha ilinijia akilini mwangu ya muundo wa hina unaofunika upara wangu!!! Ningeweza kufanya kitu maalum na tofauti, kusherehekea utamaduni kwa kutumia turubai inayopatikana kwangu kwa urahisi! Nilifurahishwa sana na wazo hilo hata sikuweza kurudi kulala. Misha aliniunganisha na Sabeen, na tulikuwa njiani kufanikisha...” Binti huyo wa gavana wa Kisumu alielezea kwa furaha.

Lupita alifichua kwamba mchoraji huyo wa hina hakuwa amewahi kufanya michoro ya hina kichwani hapo awali na kwake ndio ilikuwa mara ya kwanza.

“Sabeen alikuwa kamwe hajawahi fanya michoro ya hina kwa kichwa kabla; Sikuwahi kufanya kitu kama hicho hapo awali. Hoja yangu pekee kwake ilikuwa kwamba nilitaka kuchorwa hina ya kilele cha mjane,” Lupita alielezea jinsi michoro hiyo ilivyofanikishwa kichwani mwake.