Mustafa akutana na CS Namwamba, awashukuru watu kwa kumkung'uta mavumbi

Mustafa alisema walijadili jinsi mradi wa Talanta hela utawafaidi wasanii na pia kuonesha shukurani zake sufufu kwa wote waliomkwamua kifedha.

Muhtasari

• Baada ya kuchangiwa msaada wa Zaidi ya shilingi milioni moja, Mustafa ameibuka na muonekano mpya.

• Mustafa alijadili mengi ya waziri Ababu Namwamba katika ofisi yake na kujadili mengi kuhusu mradi wa Talanta Hela.

Mustafa akutana na CS Ababu Namwamba katika ofisi yake.
Mustafa akutana na CS Ababu Namwamba katika ofisi yake.
Image: Instagram

Katika maisha, Mungu akiamua ni wakati wako kuondokewa na shida na matatizo, hakuna mwenye uwezo wa kufungia nuru ya mwanga wako.

Msanii Mustafa ambaye wiki mbili zilizopita alikuwa akihangaika kaitka kazi ngumu za Mjengo, sasa hivi ni mtu mwingine tofauti kabisa ambaye ameonekana kujirudi katika ubora wake baada ya kutiwa nguvu za magotini na wakenya wahisani.

Baada ya kuchangiwa msaada wa Zaidi ya shilingi milioni moja, Mustafa ameibuka na muonekano mpya kabisa akiwa na bashasha usoni na safari hii alikutana na waziri wa vijana, michezo na utamaduni, Ababu Namwamba.

Mustafa kupitia ukurasa wake wa Instagram alipakia rundo la picha akiwa katika ofisi ya Namwamba ambapo alidokeza kwamba walikuwa na mazungumzo marefu yenye tija kuhusu jinsi Sanaa ya vijana itainuliwa.

“Halo watu wangu. Nilikutana na Waziri mkubwa Ababu Namwamba.Tulijadili mambo mengi jinsi tunavyoweza kuleta uhai katika tasnia yetu ya ubunifu nchini Kenya. Mara nyingi ya kutia moyo na maneno ya Busara kutoka kwa Waziri Ababu na Ps Ismail. Kutokana na ufahamu wao #TalantaHela ni ndoto iliyotimia. kwamba wasanii wa Kenya watafaidika na Sanaa yao,” Mustafa mwenye furaha na tabasamu pana kwenye uso wake alisema.

Msanii huyo pia hakusita kuwashukuru mashabiki wake na wahisani wema wote waliokwenda nje ya ndani ya mifuko yako na kumpa msaada wa kifedha baada ya video akiwa katika hali duni ya kimaisha kuvujishwa mitandaoni.

"Baraka kwenu watu wangu wazuri na Mungu awabariki nyote" Mustafa alisema kwa unyenyekevu.

Awali baada ya Mustafa kukiri kwamba video hiyo ilikuwa yake na hukuwa anafukuzia kiki, alisema kwamab mambo yake yalikwenda mrama baada ya mamake kugundulika kuugua saratani.

Mustafa alisema kuwa alilazimika kutumia hela zake nyingi katika kikimu matibabu ya mamake na ndivyo alivyojipata amefilisika na kwa kutotaka kuwasumbua watu akitaka msaada, alizamia kazi za mjengo.

Baada ya kukabidhiwa msaada wa kifedha Zaidi ya milioni moja, Mustafa alisema kuwa jambo la kwanza angelifanya ni kumaliza kumjengea mamake nyumba ambayo iliishia njiani na pia kutimiza ndoto ya mamake ya muda mrefu ambayo amekuwa akitaka kwenda Mecca, mji mtakatifu Zaidi kwa waumini wa Kiislamu huku Saudi Arabia kwa ajili ya kuhiji.