Octopizzo amsihi Rais Ruto kupunguza bei ya mafuta taa

Jumatatu, Mamlaka ya usimamizi wa nishati na petroli (EPRA) ILiliongeza bei ya bidhaa hio kwa shilingi 15,19.

Muhtasari

•Ombi hili linajiri baada ya mamlaka ya kudhibiti kawi na petroli (EPRA) kuongeza bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa shilingi 15.19.

• Aliongeza kuwa bado watu wa eneo la Kibra wanatumia mafuta taa kupika na pia wazazi wanatumia taa za koroboi ili wanao waweze kusoma.

Msanii wa kuchana mistari ya muziki Octopizzo
Msanii wa kuchana mistari ya muziki Octopizzo
Image: Instagram//Octopizzo

Msanii Eric Ohanga almaarufu Octopizzo amemsihi Rais William Ruto kupunguza bei ya mafuta taa.

Ombi hili linajiri baada ya mamlaka ya kudhibiti kawi na petroli (EPRA) kuongeza bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa shilingi 15.19.

Octipizzo ambaye amewahi kuteuliwa katika tuzo za Grammy, katika akaunti yake ya Instagram alimuomba Rais kupunguza bei ya mafuta taa ambayo kulingana naye hutumika sana na watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda.

“Wasee wanateta juu ya mafuta taa, mafuta taa imeongezwa sana na sijaskia mbunge yeyote akizungumzia hili.” alisema Octopizzo.

Aliongeza kuwa bado watu wa eneo la Kibra wanatumia mafuta taa kupika na pia wazazi wanatumia taa za koroboi ili wanao waweze kusoma.

“Hii ni ombi tu kwa bwana rais, unatuumiza juu huku bado tunapika na stovu na taa za koroboi, unaeza ongeza bei ya petroli na dizeli lakini si mafuta taa” Octopizzo aliongeza.

Bei ya mafuta taa imepanda hadi shilingi 161.13 mjini Nairobi kutoka shilingi 145.23.