Pasta Mgogo ataja sababu mbili za kuzuia wanaume kutochepuka katika ndoa

Mgogo alisema wanaume wengi wanapopata jeuri ya pesa, pepo la kutaka kutongoza wanawake wengine nje ya ndoa hupiga hodi kwao.

Muhtasari

• Mchungaji huyo alisema kwa kifupi mwanamume ni kiumbe ambacho hakiwezi ridhika hata utuame vipi.

Mchungaji Mgogo ataja sababu za wanaume wasiotaka kusaliti wake zao.
Mchungaji Mgogo ataja sababu za wanaume wasiotaka kusaliti wake zao.
Image: Instagram

Mchungaji maarufu kutoka Tanzania, Daniel Mgogo ameorodhesha sababu mbili kuu ambazo zinaweza kumfanya mwanaume asimsaliti mpenzi wake katika ndoa na kuchepuka.

Katika video ambayo Mgogo alipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram, alielezea sababu kuu ambazo zinawafanya wanaume wengi kutulia kwenye ndoa na wake zao.

Moja ya sababu ambayo Mchungaji Mgogo alitaja ni kuwa na hofu ya Mungu au wale ambao hawana pesa, aghalabu huwa watulivu sana kwenye ndoa zao na uaminifu kwa wake zao huwa katika kiwango cha haiba iliyotukuka.

“Ukiona mwanamume ana mke mmoja na ametulia naye, ni mambo mawili tu yamemfanya kutulia; moja dini imemuingia sana kiasi kwamba anaogopa kukengeuka na sababu ya pili ni hana hela,” Mgogo alisema.

Mchungaji huyo alisema mwammume yoyote anaweza kupitia changamoto za kujaribiwa na wanawake, wakiwemo wachungaji kanisani pia.

“Hata sisi wachungaji hupitia majaribu kama hayo kwa sababu mle kanisani kuna mabinti wengi ambao hawajaolewa, kwa hiyo usipokuwa na kujihimili mwenyewe, unaenda na maji. Dhambi hii haijali wewe ni mchungaji wewe ni mshirika, almaradi wewe ni kiumbe itakupata tu,” mchungaji huyo alieleza.

Mchungaji huyo alimaliza akisema kwamba kwa kawaida mwanamume ni kiumbe kisichoridhika.

Wiki chache zilizopita, mchungaji huyo pia alisema kuwa wanawake wengi wanaishi maisha marefu kuliko wanaume kwa sababu wao ni viumbe wanaopenda kuzungumza sana.

Mgogo alisema kuwa kitendo cha wanawake kuongea hutoa sumu miilini mwao wakati wanaume wengi hujinyamazia na shida zao na hilo huzaa sumu miilini kusababisho vifo vyao mapema.