Stevo ahisi majama kumpa ushindani mkali kwa mpenzi mpya, asema bila Mungu hatatoboa!

Stevo alimtambulisha mrembo huyo licha ya kumtambulisha mrembo mwingine kwa jina Grace kama mke wake katika mazishi ya babake miezi michache iliyopita.

Muhtasari

• Mrembo huyo alimtaka kuchagua mmoja kati yake au Pritty Vishy akidai kwamba bado Stevo ana hisia kwa mwanablogu huyo wa YouTube,

Stevo SImple Boy adai kuwepo ushindani kwa mpenzi wake mpya
Stevo SImple Boy adai kuwepo ushindani kwa mpenzi wake mpya
Image: Instagram

Saa chache tu baada ya msanii Stevo Simple Boy kumfichua na kumtangaza mpenzi wake mpya, msanii huyo kutoka Kibera amejitokeza mitandaoni akiashiria kwamba huenda kuna wanaume wengi ambao wamo mbioni wakimpa ushindani katika huba la mrembo huyo mpya.

Jumapili Stevo Simple Boy alipakia picha ya mrembo huyo mwenye haiba iliyotukuka na kuweka wazi kwamba ni ‘chombo’ kipya kabisa, hata baada ya kudai kwamba alikuwa na mwanamke kwa jina Grace ambaye hadi alimtambulisha katika mazishi ya babake miezi michache iliyopita.

Stevo alimtambua mrembo huyo kwa jina Trisha Khalid na kummwagia makopakopa ya emoji za mapenzi huku mrembo naye akiparamia pale kwa kutupa makopakopa kama hayo.

Stevo baada ya kuhisi kuwepo na ushindani mkali kutokana na uzuri wa mrembo huyo, alikwenda kwenye Instastory yake na kuandika kwamba Bila Mungu haoni akitoboa.

“Bila Mungu sitoboi,” Stevo aliandika.

Hilo linakuja saa chache baada ya kushiriki kipindi cha moja kwa moja na mrembo mpya ambaye alikuwa anamtaka kuchagua kati yake na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy.

Katika video hiyo, Khalid alihisi kwamba Stevo angali bado ana hisia kwa Vishy na kumtaka kufanya uamuzi wa moja la kusimamia kati yake ama mwanablogu Vishy.

"Waambie kama upo na mimi au Vishy. Ninawezaje kuwa na wewe na tunawezaje kuwa kwenye uhusiano ikiwa anaendelea kutoa maoni kwenye post zako?" mrembo huyo alimuuliza.

Stevo kwa weledi mkubwa na maneno yaliyotiliwa kwenye mizani, alimjibu kwamba kwa wakati huu yuko na yeye na huyo Vishy anayemzungumzia ni mtu aliyeahaulika.