Tanasha Donna afunguka ukweli kuhusu kuhisiwa kupata mpenzi mpya Mnigeria

Licha ya kudekezana kwa maneno na beti za mahaba, Tanasha alikanusha kuwa hakuna kitu kinaendelea zaidi ya urafiki tu.

Muhtasari

• Tanasha ana mtoto mmoja na Diamond Platnumz lakini baada ya kuachana naye takribani miaka 3 iliyopita, hajawahi muonesha mpenzi mpya.

Tanasha akanusha kuwa na mpenzi mpya
Tanasha akanusha kuwa na mpenzi mpya
Image: Instagram

Mtangazaji na mwanamuziki Tanasha Donna ameibua gumzo tena kuhusu picha aliyoipakia ya mwanamume mmoja anayedhaniwa kuwa raia wa Nigeria wiki saba zilizopita.

Tanasha alilazimika kunyoosha maelezo baada ya blogu moja ya humu nchini kuchokonoa picha hiyo na kudai kwamba wengi wa wafuasi wa Tanasha wamekuwa wakihisi ndiye mpenzi wake mpya.

Katika picha hiyo, Tanasha alikuwa amemwagia makopakopa mwanamume huyo huku akisema kuwa asingeweza kuwa na subira Zaidi kama hajamuona, maneno ambayo jamaa huyo alimjibu kwa mahaba huku akimtaja waziwazi kama mpenzi wake.

“Jiangalie, nina fahari sana kwako, hivi karibuni nitakuja Mungu akiridhia,” Tanasha aliandika.

“Mpenzi wangu Tanasha Donna nashukuru, nina hamu sana ya kupatana nawe tena,” Jamaa huyo kwa jina Zpxnso kwenye Instagram aliandika.

Hata hivyo baada ya watu kuhisi wanatoka kimapenzi, mama huyo wa mtoto mmoja alijitokeza wazi na kukana akisema kuwa ni rafiki tu na watu wasiwe wanakweza vitu vidogo kuwa vikubwa.

“Hapanaa, acha hizo sisi ni marafiki,” Tanasha alisema.

Wiki mbili zilizopita, msanii huyo ambaye ni mzazi mwenza wa Diamond Platnumz kutoka Tanzania aligonga vichwa vya habari alipodokeza kuwa hana furaha kuishi nchini Kenya na kuwa alikuwa na mpango wa kuhama kabisa pamoja na mwanawe kwenda nchi za mbali.

Tanasha alisema kuwa habari mbaya kila uchao nchini zilimfanya kujihisi hayuko katika mazingira salama kabisa kwake na mwanawe.