Uwe na hatia au la, jaribu sana kujizuia dhidi ya kuzungumzia kifo cha Jeff - Fatxo ashauriwa

Nyoro alimshauri kwamba kuendelea kuzungumzia kifo cha Jeff kunawaathiri pakubwa familia ya marehemu ambao bado wana machungu ya kufiwa.

Muhtasari

• Nyoro alimsihi Fatxo kukwepa kabisa kuruhusu mazungumzo yoyote yanayolenga kubaini jinsi Jeff alifariki.

• Alimwambia kuwa ikiwa ni kuzungumza basi ajizungumzie mwenyewe na kaika kuzungumza asiwe kama anajitetea kwani ukweli siku zote hauhitaji kutetewa sana.

Fatxo ashauriwa kuepuka kabisa kujadili suala la kifo cha Mwathi Jeff.
Fatxo ashauriwa kuepuka kabisa kujadili suala la kifo cha Mwathi Jeff.
Image: Facebook

Kufuatia mahojiano yake ya kipekee na kituo cha Radio Jambo amabyo pia yalikuwa yake ya kwanza kabisa tangu sakata la kifo cha Jeff, Mcheza santuri DJ Fatxo amevutia hisia mseto mitandaoni.

Baadhi ya watu wamejitokeza kumkashifu kwa kufanya mahojiano hayo kunyoosha maelezo kufuatia kuhusishwa na kifo cha Jeff huku wengine wakisimama naye kwamba ni vizuri kujieleza ili Wakenya pia wajue kuhusishwa kwake na kifo hicho.

Ndungu Nyoro, mkurugenzi mkuu wa wakfu wa Affecto ni miongoni mwa wale waliomshauri Fatxo dhidi ya kuzungumzia kwa njia yoyote mazingira ya jinsi Mwathi alifariki, iwe ana hatia au la.

Kulingana na Nyoro, Fatxo kuendelea kuzungumza kwenye media kufanya mahojiano kuhusu suala hilo sit u kunamchafua bali pia kunawaumiza wanafamilia wa Jeff ambao bado wanaomboleza kifo cha ghafla cha mpendwa wao.

“Lakini ningependa ufahamu hili. Familia moja ilimpoteza mtoto wao wa kiume. Na wanaumia. Jeraha bado ni mbichi na linaweza kuchukua muda kupona. Iwe una hatia au huna hatia, epuka suala hilo kabisa. Ni suala la hisia. Epuka kuburutwa kwenye mazungumzo ambayo yana uwezekano wa kujadili au kuhalalisha ni nani alifanya nini katika usiku wa maafa. Epuka kumtaja Jeff. Epuka kuwataja jamaa zake. Epuka kabisa. Achana na mada hiyo kabisa,” Nyoro alitema lulu kwa Jeff.

Katika suala la Jeff, unaweza kuwa hauna hatia au hatia. Ni Mungu tu, shetani, Jeff, marafiki uliokuwa unawakaribisha usiku ule, na wewe mwenyewe ndio unaojua ukweli. Ukweli mtupu, alisema.

Mkurugenzi huyo wa wakfu wa kufadhili masomo ya watoto kutoka familia zisizojiweza alimshauri Fatxo kuacha suala hilo kwa marafiki zake ikiwa wapo kulijadili na media na wala si yeye mwenyewe kufanya hivyo.

“Ikiwa unapaswa kujadili chochote, jadili kuhusu wewe mwenyewe. Jadili kuhusu kuvunjika kwako kihisia, uponyaji au chochote kinachotokea. Jadili kuhusu viwango vya juu na vya chini. Na unaweza kufanya hivyo bila kujitetea. Ukweli hauhitaji kutetewa sana. Ina njia ya kujidhihirisha yenyewe, kwa wakati wake.”