Gidi: Kwa nini mawasiliano ya FB ni magumu haswa ukiwa na hadhara mchanganyiko

"Wakati fulani unataka kujihusisha na mada fulani yenye kuchochea mawazo lakini kuna sehemu ya wasikilizaji wako watafikiria unawadharau." - Gidi.

Muhtasari

• Mtangazaji huyo alisema hali kama hii haipo kwenye WhatsApp kwani kule hadhira ni maalum kwa sualaFulani.

Mtangazaji Gidi Ogidi

Mtangazaji wa Radio Jambo katika kipindi cha asubuhi Gidi ameelezea chanzo cha ugumu wa mawasiliano ya mitandaoni haswa Facebook baina ya watu maarufu na wafuasi wao.

Gidi anahisi kwamba wakati mwingine watu wenye umaarufu mkubwa mitandaoni huwa na ugumu kufanya mawasiliano ya maana na wafuasi wao kwani mara nyingi watu hawa huwa na ufuasi wa watu kutoka kila tabaka.

Gidi alisema kwamba haswa yeye hupata wakati mgumu kuwaelewesha wafuasi wake kwani hadhira yake imechanganyikani matabaka na wakati mwingine akijaribu kuzungumzia kitu cha mzaha huwa anapoteza hadhira ya watu wasomi na wakati mwingine pia akiamua kuzungumzia kitu cha kitaaluma huwa anawapoteza wale wapenda mzaha – hivyo kuleta mkwamo mkubwa katika mawasiliano.

“Mawasiliano kwenye Facebook yanazidi kuwa changamoto, haswa ikiwa una hadhira iliyochanganyika ya umma. Wakati fulani unataka kujihusisha na mada fulani yenye kuchochea mawazo lakini kuna sehemu ya wasikilizaji wako ambayo itapotea, wengine wanaweza hata kufikiria kuwa unawanyanyasa au kuwadharau,” Gidi alihisi.

“Halafu saa zingine pia uko tu na stories za mtaa, za ma hustlers ama za spoti hivi, halafu unajikuta tena unapoteza sehemu nyingine ya watazamaji wako ambao wanaona chapisho lako ni la kina sana au halijafikia viwango vyao. Hili ni tatizo la mawasiliano pengine mahususi kwa jukwaa la Facebook.”

Mtangazaji huyo alisema hali kama hii haipo kwenye WhatsApp kwani kule hadhira ni maalum kwa sualaFulani lakini katika Facebook hadhira huwa imechanganyikana kutoka kila tabaka.

Gidi alielezea kuwa baada ya kujua hilo kwenye Facebook, ndio maana amejikita sana katika kuzungumzia masuala yote kutoka siasa, utani, spoti na mengine ya kawaida.

“Ndiyo maana huwa napenda kushikilia mada za jumla kuhusu kashfa za michezo, habari laini, kejeli au vicheshi tu vya mtandaoni. Facebook sio jukwaa la mazungumzo ya mada ya kina,” Gidi alisema.