Msanii wa nyimbo za bongofleva kutoka Tanzania Yusuf Kilungi maarufu Mbosso amefunguka kuhusu mzozo unaodaiwa kuwepo kati yake na Marioo.
Kulingana naye, kila msanii hasa katika Wasafi anapokuwa na jambo au sherehe huwaalika wengine hivi kwamba iwapo hujaalikwa huwezi kuhudhuria kwa hofu ya kuzuiliwa mlangoni au aibu yoyote ile.
Licha ya wasanii wengi wa Bongo kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa albamu ya Marioo mapema mwaka huu, Mbosso hakuonekana pale na katika mahojiano na Wasafi Media aliombwa kueleza kwa nini hakuhudhuria.
“Hivi leo nataka niweke kila kitu sawa.Mimi huwa sina unafiki maana humwaalika kila mtu katika jambo langu na hasa watu wanaotuweka katika picha tofauti, pia huwaalika ndipo waone sisi hatuna shida,” alisema.
Mbosso aliendelea kusema kuwa,alimkaribisha Marioo alipokuwa akizindua IP yake, na pia aliposti kwenye ukurasa wake licha ya kuongea naye binafsi, lakini kwake yeye Marioo hakumjulisha kuwa angekuwa akizindua jambo fulani au albamu mpya.
“Mimi kwenye shoo yake hakunialika,au hata kuniposti labda ningeona mwaliko huo kwenye mitandao na kuhudhuria. Kwenye baadhi ya picha zilikuwa na logo, ya Diamond ilikuwa na logo ikiwa na maana ndiye pekee alikuwa amelikwa” Alisisitiza kuhusu kutohudhuria kwake.
Mbosso anayeendelea kushamiri kutokana na mdundo wa nyimbo zake alitia sahihi na shirika kuu Afrika la kurekodi nyimbo WCB Wasafi tangu mwaka wa 2017 kuendeleza kipaji chake.