Msanii rapa wa Bongo Fleva Nay wa Mitego ameachia kazi mpya akimshirikisha msanii Linah Sanga na tayari video ya ngoma hiyo kwa jina ‘Mshua’ imepakiwa YouTube.
Video hiyo imegeuka kuwa gumzo kubwa haswa baada ya baba yake na Diamond Platnumz, Mzee Abdul akiigiza kama ‘video King’ – jambo ambalo limewaacha wengi wakizungumza maana ya Nay kumtumia mzee wa Diamond kwenye video yake.
Kwa muda mrefu mzee Abdul alikuwa anafahamika na wengi kama babake Diamond kabla ya miaka ya hivi karibuni mama Dangote kuweka wazi kuwa siye baba wa kumzaa Diamond, akijaribu kuteua kitendawili kuhusu ni kwa nini msanii huyo licha ya kunukia utajiri hajawahi msaidia mzee huyo.
Mzee huyo aliwahi fanya mahojiano akisema kuwa anaugua saratani ya ngozi lakini hakuna mtu kutoka kwa wale aliokuwa akiwaita familia yake – kwa maana ya mama Dangote na mwanawe Diamond, hawakuwahi kumpa msaada wowote.
Kilichoibua gumzo pevu kuhusu video hiyo hata hivyo ni mada na maana ya wimbo huo ambao umejikita Zaidi katika kuzungumzia mateso na shida ambazo baba anapitia kuhakikisha kwamba familia yake iko sawa kwa kila kitu lakini mwisho wa siku anageuzwa kuwa zulia la kukanyagwa tu.
“Kwenye familia wewe ndio kichwa na tuliona ulivyopambana lakini mimi na wadogo zangu tulisema hivi nani kama mama,” sehemu ya mishororo kwenye shairi hilo la Nay wa Mitego iliimba.
Sasa hiki ndicho kimewafanya baadhi wahisi kwamba Nay alikuwa anatupa bomu la moto kwa Diamond na mama yake kwa kumtelekeza mzee wake licha ya kujitoa pakubwa kiasi msanii huyo alikuwa mdogo.