Baada ya kutumbuiza Kombe la Dunia, Rais wa 'World Bank' alimpa babangu kazi - Davido

"Babangu ana marafiki wengi wenye haiba ya juu lakini kwa muda mrefu alikuwa amejaribu kukutana na rais wa dunia bila mafanikio. " - Davido.

Muhtasari

• Davido alisema baada ya kumaliza kutumbuiza alielekea kweye chumba chake na kukutana na Malpass, rais wa benki ya dunia.

• Aliposalimiana naye mara alimpigia babake simu na kumpa wazungumze naye, hivyo kufanikisha ndoto ya mzee wake.

Davido aeleza jinsi aliwakutanisha babake na rais wa benki ya dunia
Davido aeleza jinsi aliwakutanisha babake na rais wa benki ya dunia
Image: Instagram, Maktaba

David Adeleke almaarufu Davido, msanii wa Nigeria aliyeshinda tuzo nyingi, amefichua kwamba alimuunganisha babake, Bw Adedeji Adeleke, na Rais wa Benki ya Dunia David Malpass.

Davido alisema kwamba aliweza kumuunganisha babake tajiri na Malpass wakati wa mkutano mfupi kwenye Kombe la Dunia la 2022 huko Qatar.

Katika mahojiano na mwanahabari maarufu wa Marekani Big Boi, mwimbaji huyo wa ‘Fall’ alifichua kuwa babake amekuwa akijaribu kuonana na rais wa Benki ya Dunia kwa muda lakini hakuwa amebahatika kufanikisha hilo.

Msanii huyo alisema kuwa baada ya kufanya sherehe za kufunga Kombe la Dunia, alikutana na Malpass kwenye hoteli yake, na mchambuzi wa uchumi alisifu jinsi Davido alivyoliteka jukwaa la utumbuizaji wake uliowakosha wengi.

Alidai kuwa mara baada ya kupeana salamu za furaha na Malpass kujitambulisha, aliwasiliana na baba yake na kumweleza kuwa anakutana na Rais wa benki hiyo ya dunia nzima.

Aliposema hivyo, baba yake alimwomba ampe simu Malpass, na hivyo ndivyo walivyounganishwa kwa mpango na kijana huyo.

Davido alisema; "Baba yangu ana marafiki wengi mahali pa juu na amekuwa akijaribu kumtafuta rais wa benki ya dunia. Amekuwa akijaribu kufika kwa rais huyo na rais huyo alikuwa kwenye kombe la dunia. aliniona hotelini na kusema “Davido nimefurahia utumbuizaji wako, mimi ni Rais wa Benki ya Dunia”, nikasema; “Shika “hello baba, nina rais wa benki ya dunia” akasema; “Mpe simu”, aliunganisha mpango hivyo hivyo.

Tumbuizo lake kwenye kufunga sherehe za kombe la dunia Desemba mwaka jana zilikuwa za kwanza kabisa kwake kuonekana hadharani baada ya kuwa mbali na kamera kwa Zaidi ya mwezi mmoja kufuatia kifo cha ghafla cha mwanawe wa pekee, Ifeanyi.

Inaarifiwa kwamba Davido alikuwa ameratibiwa kutumbuiza katika sherehe za ufunguzi wa kampeni za kombe la dunia lakini mwanawe alifariki siku chache kuelekea kipute hicho, jambo lililomfanya kughairisha shughuli zote alizopangiwa kufanya kwa mwezi Novemba na Desemba.

Msanii huyo hata hivyo amerudi mwaka huu kwa vishindo vya kutisha ambavyo aliachilia albamu yake yenye nyimbo 17, Timeless na ambayo inazidi kupata mapokezi ya kishujaa.