Esther Musila: Maisha yangu yalianza Guardian Angel aliponipenda nikiwa miaka 50

Kwa wengi, maisha huanza katika umri wa miaka 40, lakini kwa Musila, mama wa watoto 3 mwenye miaka 53, maisha yake yalianza akiwa miaka 50 alipokutana na Guardian Angel.

Muhtasari

• Mama huyo wa watoto watatu alimfurahia mpenzi wake Guardian Angel na kusema kuwa maisha yake yalikuwa yamegoma lakini yalianza alipompenda.

Guardian Angel amsherehekea mpenzi wake
Guardian Angel amsherehekea mpenzi wake
Image: Instagram

Kuna kauli mitaani na mitandaoni kuwa maisha huanza rasmi kwa watu wengi pindi wanapofikisha miaka 40, lakini kwa Esther Musila ambaye ni mpenzi wa msanii wa injili Guardian Angel, maisha yake yalianza rasmi alipofikisha miaka 50.

Musila alidokeza hili Alhamisi Mei 24 wakati alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa akifikisha miaka 53.

Wakati anasherehekea kufikisha miaka 53, pia alikuwa anasherehekea miaka 3 tangu walipokutana na kujuana na mpenzi wake Guardian Angel na kusema kwamba maisha yake yalianza kipindi hicho akiwa na miaka 50.

Mwanamama huyo alimpongeza Angel mwenye umri wa miaka 35 kwa kumkubali licha ya pingamizi nyingi kutoka kwa jamii kuhusu kigezo cha utofauti mkubwa kiumri baina yao.

"Maisha yangu yalianza nilipokutana na wewe mpenzi wangu, imekuwa miaka 3 ya furaha na nakushukuru kwa kuja. Ulileta maana mpya kabisa kwa uwepo wangu. Nakupenda Mfalme wangu,” Musila alimwandikia mpenzi wake kwa furaha baada ya Angel kumsherehekea kwa ujumbe wa kutamanisha.

Penzi la wawili hao limekuwa likiwekwa kwenye mizani ya umma na wengi, wakihisi kwamba msanii wa injili amefumbwa macho kupendana na Musila ambaye mtoto wake wa kwanza ni karibia umri wa Angel.

Baadhi wanahisi kwamba wawili hao hawatafanikisha lengo la familia na ndoa halisi – kupata watoto, kwani Musila tayari umri wake umeshakwenda sana, lakini wamewahi jitokeza wazi mara kadhaa na kukanusha kwamba mapenzi yao yanalenga katika kupata watoto.

Musila aliwasuta vikali waliokuwa wakimtaka kumzalia Angel Mtoto akisema kuwa maisha yake na mpenzi wake hayafai kuingiliwa na watu kwa njia yoyote ile, achia mbali kuratibiwa cha kufanya kwani hata wapate watoto jinsi jamii inavyowashinikiza, haitawapa msaada wowote katika kuwalea.

“Watoto ni baraka kutoka kwa Mungu. Mtoto ni bonasi...tukipata ni sawa, kama sivyo bado tutapendana. Ikiwa nilioa mwanamke mdogo na kwa sababu moja au nyingine akashindwa kupata mimba, itakuwa sawa kuondoka? Je, yeye pia aondoke ikiwa siwezi kuzaa watoto?" aliuliza Guardian kwa kipindi kimoja kwenye mahojiano.