Marioo amuomba Mbosso msamaha kwa kum'snitch," Nisamehe, wewe ni mtu wa Mungu!"

Mbosso alisema kuwa Marioo alikuwa anakwenda kwenye mahojiano na kumchafulia picha lakini akirudi kwake anamsalimia kama rafiki kabisa.

Muhtasari

• Mbosso alisema kuwa alimwambia wazi wazi kuwa huo ni unafiki na siku zote mtu mnafiki hawezi kuwa kwenye mduara wa marafiki zake na akaamua kumpotezea Marioo.

• “Wewe ni ndugu yangu bwana Kirungi (Mbosso), hatuna sababu ya kugombana sababu sisi wote ni wanadamu." - Marioo.

Marioo amuomba Mbosso Msamaha.
Marioo amuomba Mbosso Msamaha.
Image: Instagram

Baada ya Mbosso kufunguka kuwa Marioo ana chuki naye ambayo haijulikani chanzo chake ni kipi, hatimaye Marioo amejitokeza mazima na kumuomba msamaha Mbosso huku akimtaka waketi wayajenge wote kama wasanii wachanga.

Katika kipindi cha Refresh kwenye kituo cha Wasafi TV, Mbosso alifunguka kuwa Marioo alimzungumzia mabaya kwenye mahojiano lakini walipokutana Marioo akamsalimia na hao ndipo Mbosso aliamua kumvaa akitaka kujua mbona alikuwa anamchafua kwenye Mahojiano lakini kufika kwake akajivika joho la utakatifu.

“Tunakutana uwanjani na tunasalimiana na mwisho juzi katoka kwenye mahojiano nimemuona kabisa na alichokionge nilikiona kabisa, kanikuta uwanjani pale kanipa mkono na nikakubali freshi lakini nikamuuliza mbona ukija hapa unanisalimia lakini ukikaa kwenye mahojiano unaniongelea vibaya ili wewe uonekane mzuri na mimi nionekane mbaya,” Mbossi alisema kwenye kionjo hicho cha mahojiano.

Alisema kuwa alimwambia wazi wazi kuwa huo ni unafiki na siku zote mtu mnafiki hawezi kuwa kwenye mduara wa marafiki zake na akaamua kumpotezea Marioo.

Baada ya Marioo kusikia maneno ya Mbosso kuwa amemtoa kwenye orodha ya mrafiki zake, alipakia video hiyo ya mahojiano kwenye instastory yake akionekana kuwa gym na alichokifanya ni kuomba radhi kwa Mbosso.

“Wewe ni ndugu yangu bwana Kirungi (Mbosso), hatuna sababu ya kugombana sababu sisi wote ni wanadamu. Tunatafuta riziki na tunamuomba Mungu mmoja. Kama kuna kitu kimetokea si kizuri, tusimkaribishe shetani, tusameheane ndugu yangu, acha tufanye kazi bila kuwa na hisia za kero kwa mwingine. Mungu akubariki,” Marioo alisema kwenye video hiyo.

Marioo alizidi akimtawaza Mbosso kuwa ni mtu wa Mungu na kumtaka asamehe yaliyotokea awali na kufanya kazi kama vijana ambao wote wanasakanya mpunga.

 Kwa kumuita kwa jina lake la ukoo – Kirungi – inaonesha ni jinsi gani Marioo alikuwa anamaanisha katika msamaha wake na si utani ule wa kisanaa.

Inasubiriwa kuonwa kama Mbosso ataridhia msamaha wa mwenzake na kuamua kuyapiga pasi au atazidi kumkandia.