Msanii Nadia Mukami kwa mara ya kwanza amezungumzia kitu kilichosababisha kukosana na mume wake ambaye pia ni msanii mwenzake, Arrow Bwoy.
Akizungumza na mtangazaji wa Radio Jambo, Massawe Japanni, Nadia alisema kuwa kipindi alifichua mitandaoni kuwa hawakuwa pamoja tena alikuwa anamaanisha na wala si kiki kama ambavyo wengi walihisi.
Wasanii hao wawili ambao walikuwa studioni kutambuliza kazi zao mpya walisema kuwa walikosana tu lakini haikuchukua muda mrefu kabla ya kurudiana.
Kwa upande wake, Arrow Bwoy alisema kuwa ni kawaida yake kuondokea zogo linapotokea na ndio maana aliamua kujichomoa katika nyumba hiyo ili kujipa nafasi ya kutuliza na kunyoosha maelewano kabla ya kurudi.
Nadia alisema kuwa baada ya Arrow Bwoy kuondoka, alijirudisha tu mwenyewe wala hakumuomba msamaha.
“Nafikiri wanaume Waluhya hawajui kuomba msamaha. Aliondoka na kurudi bila kuomba msamaha. Aliakuwa anarudi akijifanya kuwa ni kuuliza mtoto anaendelea aje. Anapenda sana mtoto wake,” Nadia alisema kaitka mahojiano hayo.
Arrow Bwoy alisema kuwa alirudi hata Nadia naye hakumuomba msamaha na baadaye walipata mwafaka baada ya kuketi chini ya kumsikiliza kile ambacho alikuwa anapitia baada ya kujifungua.
Kai alikuwa ni mtoto wao wa kwanza kwani si Nadia wala Bwoy ambaye alikuwa amewahi kupata mtoto mwingine na msanii huyo wa kike alimsifia pakubwa Arrow Bwoy kwa kumuonesha mapenzi ya kudumu haswa kipindi cha mwanzo kabisa alipojifungua.
“Mimi namshukuru sana Arrow Bwoy kwa sababu nilipojifungua alikuwa ananifanyia kazi zote mpaka kupika. Pia anaonesha mapenzi ya kudumu na yenye haiba ya juu kwa mtoto wetu Kai na siwezi kuomba kupata baba mwingine kwa mtoto wangu kando na yeye,” Nadia alisema.
Wawili hao walikuwa studioni kupigia debe albamu yao ya Love and Vibes.