Upasuaji wa Tanasha Donna ulinigharimu sana- Risper Faith

Kulingana na Risper Faith Upasuaji wa kumwongezea Tansha makalio ulimuathiri pakubwa.

Muhtasari

• Risper pia alidai kuwa Tanasha alishindwa kupata huduma ya baada ya upasuaji, ambayo inaweza kuhatarisha afya yake na kupona.

• Tanasha alisisitiza kuwa tuhuma hizo zilikuwa za uongo na kuwa hazikukuwa na ushahidi wowote.

Tanasha Donna na Risper Faith.
Tanasha Donna na Risper Faith.
Image: INSTAGRAM

Risper Faith amefunguka kuhusu kile alichopitia baada ya kumtambulisha Tanasha Donna kwenye kliniki ya upasuaji wa kuongeza urembo ambayo alidai ilimsababishia matatizo kadhaa.

Katika mahojiano na Mwende Macharia kwenye Radio Maisha, Risper alifichua undani wa kukutana kwake na Tanasha na matokeo ya ushirikiano wao.

Risper alieleza kuwa Tanasha aliwasiliana naye kupitia ujumbe katika akaunti yake ya Instagram, akieleza nia yake ya kufanya upasuaji wa kuongeza urembo na kutafuta ushauri wa Risper kuhusiana na hilo.

kampuni ambayo Risper alikuwa akifanya kazi nayo ilikuwa ikitafuta mtu wa kufanya upasuaji huo, hivyo akamtambulisha Tanasha kwao.

"tatizo hili na Tanasha lilinigharimu kikubwa. Ukweli ni kwamba, kampuni ilikuwa inatafuta mtu wa kufanya upasuaji wa kuongeza makalio. Na kisadfa, Tanasha alinitumia ujumbe akiniuliza ikiwa nimefanya yangu, hivyo nikamtambulisha kwao,” Risper alifichua kwenye mahojiano hayo.

Kulingana na Risper, kulikuwa na makubaliano kwamba Tanasha angechapisha taarifa kwenye mitandao yake ya kijamii kuhusu biashara ya kampuni ile, jambo ambalo Tanasha hakulifanya.

Kampuni hiyo ilifikia hata kuajiri timu ya wataalamu wa kupiga picha za video ili kurekodi  safari mzima ya kufanya upasuaji huo.

Hata hivyo, Risper alidai kuwa wiki mbili tu baada ya upasuaji, Tanasha hakufanikisha hilo.

Risper pia alidai kuwa Tanasha alishindwa kupata huduma ya baada ya upasuaji, ambayo inaweza kuhatarisha afya yake na kupona.

“Utaratibu huo uligharimu takriban shilingi 860,000. Kampuni ilikuja kunitafuta kwa sababu nilimtambulisha kwao. Hata ikawa kesi ya polisi. Hata sasa ninaweza kupoteza mkataba wangu ikiwa nitaendelea kuzungumza juu ya swala hilo. Baada ya tukio hilo, alikata mawasiliano yetu kila mahali mitandaoni,” Risper alisema.

Wakati wa mahojiano ya redio mnamo 2022, Tanasha Donna alizungumzia suala la habari za uwongo zinazosambazwa kumhusu na akakanusha madai ya wale wanaoeneza uvumi huo.

Tanasha alisisitiza kuwa tuhuma hizo zilikuwa za uongo na kuwa hazikukuwa na ushahidi wowote.

"Ninafadhaika kujibu maswali kuhusu simulizi za uwongo na porojo zisizo na msingi. Niko tayari kuzungumzia mambo ya kibinafsi, lakini nakataa kujibu maswali yanayotegemea uwongo."  alisema.