Hisia mseto baada ya Embarambamba kunengua mauno akiwa amevalia rinda na blauzi ili kujipigia debe

Embarambamba alibainisha kuwa wanawake pia huchapisha video zinazoonyesha wakitikisa viuno na makalio yao ili kujitangaza.

Muhtasari

•Embarambamba alionekana akidensi na kucheza miondoko ya kustaajabisha huku akiwa amevalia rinda fupi la kahawia na blauzi nyekundu.

•Video hizo zimeibua hisia mseto kutoka kwa wanamitandao huku wengi wao wakionekana kushangazwa na vituko vya mwanamuziki huyo.

Image: INSTAGRAM// EMBARAMBAMBA

Mwimbaji wa nyimbo za Injili kutoka Kisii, Christopher Musyoma almaarufu Embarambamba amezua mdahalo mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuonekana amevalia mavazi ya kike ili kuipigia debe chaneli yake ya YouTube.

Katika video iliyochapishwa kwenye akaunti yake ya Instagram, mwimbaji huyo aliyezingirwa na utata mwingi alionekana akidensi na kucheza miondoko ya kustaajabisha huku akiwa amevalia rinda fupi la kahawia na blauzi nyekundu.

Baba huyo wa watoto watano alisikika akiwaomba Wakenya kujisajili kwenye chaneli yake ya YouTube huku akibainisha kwamba wanawake pia huchapisha video zinazoonyesha wakitikisa viuno na makalio yao ili kujitangaza.

“Serikali ya Rutoo… subscribe Embaramba YouTube channel and share,” Embarambaramba alisema huku akicheza.

Pia alichapisha video zaidi zilizomuonyesha akicheza moja ya nyimbo zake maarufu huku akiwa amevalia nguo hizo.

Video hizo ambazo sasa hivi zimesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii zimeibua hisia mseto kutoka kwa wanamitandao Wakenya huku wengi wao wakionekana kushangazwa na vituko vya mwanamuziki huyo.

OKIS_DUNGAMAWE  Hata kama ni kusaka dooh hii imezidi jooh

Dan Angwenyi Huyu ni LGBTQ kabisa

Jane Nyabuto Napenda nchi yangu

Mercy Ramsey Aibu sana

Maxwell Gerald Kama hii ndio talent heri tukae bila

Mawanda Zeddy Wait, hiyo skirt ametoa wapi

Turn Cypher Huyu naye amechizishwa na uchumi venye uko juu.

Mwanamuziki Embarambambamba ambaye anatoka kaunti ya Kisii anafahamika kwa nyimbo zake za kutatanisha na miondoko ya densi. Nyimbo zake nyingi kwa kawaida huwa vichekesho  kwani huwa anafanya densi za kuchekesha ikiwa ni pamoja na kukimbia juu na chini na kupanda juu ya majengo na miti kisha kuruka chini.

Alianza taaluma yake ya muziki takriban miongo miwili iliyopita ila alijizolea umaarufu mkubwa mwaka wa 2021 baada ya moja ya video zake akicheza densi za kutatanisha kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.