• Kauli ya Davido ilitolewa kuangazia zao la wasanii wapya wanaopeleka Afrobeats kwa hadhira ya kimataifa kufuatia juhudi kubwa na za kuweka kasi zinazofanywa na yeye na Wizkid
Mmiliki wa kampuni ya Microsoft ambaye pia ni tajiri namba sita duniani, Bill Gates yuko nchini Nigeria wiki hii kwa mwendelezo wa kazi zake za kutoa misaada barani Afrika.
Akiwa nchini humo, mkwasi huyo alipata kuzungumzia jinsi alivyojiandaa kwa safari hiyo na kusema kuwa alimuaga binti yake Phoebe na kumwambia kwamba alikuwa anaelekea Nigeria.
Baada ya binti yake kusikia hivyo, alifurahi akimwambia baba yake kuwa angalau alikuwa katika nafasi kubwa ya kukutana na kati ya wasanii wakubwa wanaofanya vizuri kote duniani kwa miziki ya Afrobeats, Burna Boy na Rema.
Kwa mshangao, Gates alimwambia binti yake kuwa hakuwa amewasikia wawili hao hata mara moja katika maisha yake akiahidi kuwa angewatafuta, lakini wakati huo huo pia alisema kuwa yeye alikuwa anawatambua kwa kiasi kikubwa Davido na Wizkid.
“Wakati binti yangu Phoebe alisikia kwamba nilikuwa nakuja nchini Nigeria, alifurahi na kuniambia ‘una bahati kwa sababu utapata kukutana na Burna Boy na Rema’... kwa hiyo ilinibidi niwatafiti kwanza kwa sababu mimi si mtu wa hizo nyimbo, lakini nakumbuka mara ya mwisho nilikuwa hapa, niliweza kuwaona Davido na Wizkid wakitumbuiza,” Bill Gates alisema.
Kauli ya Gates imezua taharuki kwenye mitandao ya kijamii huku bilionea huyo akirudia maneno ya Davido ambaye hivi majuzi alimtaja Burna Boy kama "Paka Mpya" wakati wa mahojiano na jukwaa la vyombo vya habari vya Ufaransa.
Kauli ya Davido ilitolewa kuangazia zao la wasanii wapya wanaopeleka Afrobeats kwa hadhira ya kimataifa kufuatia juhudi kubwa na za kuweka kasi zinazofanywa na yeye na Wizkid.
Kauli hiyo iliwachanganya Wanigeria kwenye Twitter huku wakitofautiana na usahihi wa uainishaji huo huku wengine wakikubaliana na Davido huku wengine wakishikilia kuwa Burna Boy hawezi kuainishwa kama paka mpya kwani alitoa wimbo wake wa kwanza 'Like To Party' mnamo 2013.