Waliokuwa wasimamizi wa mwanamuziki Stevo Simple Boy, Men In Business wamevunja kimya chao baada ya mpenzi wa mwanamuziki huyo, Grace Atieno kudai kuwa hana udhibiti wa akaunti zake za mitandao ya kijamii na za kifedha.
Katika mahojiano ya kipekee na mwanahabari wa Radio Jambo Samuel Maina, walikanusha madai kuwa wanaendesha akaunti za msanii huyo kutoka kibra.
MIB pia walikanusha madai ya Grace kwamba Stivo hafahamu kiwango cha pesa ambacho huwa analipwa kwa kila shoo.
“Hapana stevo Simple Boy anajua kila kitu kuhusu pesa zake kwa sababu anaitia saini mikataba hizo. Ana pahali anapaswa kutia saini wakati wa kuweka mikataba kwa hivyo kwa mfano kama tunalipwa shilingi 50,000 anajua asilimia takayo pokea.” alisema aliyekuwa meneja wa Stevo.
Mke wa mwimbaji huyo anayefahamika kama Grace awali alikuwa amekiri kuwa usimamizi wa msanii huyo ulimiliki na kuendesha akaunti zake za kijamii na hata zile za benki, madai ambayo kampuni hiyo imepinga.
“Unaeza endesha aje akaunti ya benki inayomilikiwa na mtu mwingine? Benki hutumia alama za vidole nitatumia aje akaunti yake ya benki ilhali sina alama zake za vidole? Ako na akaunti zake na yeye mwenyewe anazimiliki na kuziendesha. “
Pia alikanusha vikali tetesi zilizokuwa zikienea mitandaoni kuwa wanamiliki na wanazifahamu namba za siri za akaunti ya mpesa ya mwanamuziki huyo.
“Si zifahamu neno siri za mpesa ya Stevo, sijui kabisa, nina password nyingi za kazi kushika password ya Stevo, we have all the transactions za pesa kwa akaunti ya Stevo kwa hivyo itakuwa rahisi kudhihirisha.”
Jumamosi, Grace, mke wa Stevo Simple Boy alidai kuwa usimamizi wa Stevo Simple Boy unaendeleza na kusimamia kila kitu ikiwemo akaunti zote za mitandao ya kijamii, mawasiliano na hata malipo.
“Najua watu wengi wanajua Stivo ni yeye hutumia Tiktok yake na Instagram, lakini sio yeye. Wengi huwa wanalalamika kwamba wanataka kumsaidia na kitu kidogo lakini hawamkuti. Yaani anapitia changamoto nyingi tu.. Hana akaunti yoyote anayotumia. Meneja wake ako na kila kitu chake. Hata kumpata, huwezi kumkuta kwa urahisi.”
Bi Grace alifichua kwamba mumewe ata hafahamu kiasi cha pesa ambacho huwa analipwa kwa kila shoo
“Tunapitia magumu ni ile tu huwezi kutoka nje kuomba mtu nini na nini, tunavumilia tu. Wakati mwingine tunagombana kutokana na hizo tu changamoto lakini ukimwambia aende aongee na meneja wake mambo ya hela ajisimamie mwenyewe anaogopa,” Grace alisema.