Stevo Simple Boy atangaza kujisimamia mwenyewe baada ya kutemwa na meneja

"Sai mimi nimeamua kuwa meneja kivyangu nikiwa na mke wangu na rafiki zangu watatu" alisema Stevo.

Muhtasari

• Stevo Simple Boy alibainisha kuwa sasa atajiwakilisha yeye mwenyewe akisaidiwa na mke wake na marafiki wake watatu.

• Stevo Simple Boy alifunguka na kudai kuwa meneja wake wa zamani hakuwa akimsaidia katika taaluma yake na alitumia fursa hiyo kujinufaisha.

Mwanamuziki Stivo Simple Boy
Image: HISANI

Mwanamuziki maarufu kutoka Kibera, Stevo Simple Boy amevunja kimya chake baada ya usimamizi wake, MIB kusitisha mkataba wake na kampuni hiyo na sasa amefichua kuwa atajisimamia.

Siku ya Jumatatu, mwanamuziki huyo akipokea msaada wa kifedha kutoka kwa mchekeshaji Mulamwah na ni wakati huo alibainisha kuwa sasa atajiwakilisha yeye mwenyewe akisaidiwa na mke wake na marafiki wake watatu.

“Sai mimi nimeamua kuwa meneja kivyangu nikiwa na mke wangu na rafiki zangu watatu pamoja na wakenya wote kwa jumla. Kama mtu anataka kunisupport wakuje kwangu mimi binafsi.”

Stevo Simple Boy alidai kuwa meneja wake wa zamani ,ambaye siku ya Jumatatu alikatisha mkataba wao, hakuwa akimsaidia katika taaluma yake na alitumia nafasi hiyo kumhujumu.

“Meneja hafanyi kazi nzuri, ukiangalia kwanza Instagram hapost msanii wake anapost msanii mwingine na kumpromote.”

Pia aliongeza kuwa yanayoendelea sio njia moja ya kutafuta umaarufu bali ni hali halisi kwani hajafanya shoo yoyote kuanzia mwezi wa Januari.

“Jambo la kwanza kuanzia Januari sijapiga shoo, sihitaji pesa nyingi kufanya shoo 20, 000 ama 30,000 inatosha kwangu.”

Badhi ya wakenya na wasanii wenzake katika tasnia pana ya Burudani nchini wamejitokeza kwa sauti moja na kumtetea mwanamuziki huyo ambaye wengi walihisi ni dhaifu na meneja alikuwaa akimnyanyasa.

 Licha ya tetesi za unyanyasaji wa Stevo kuenea mitandaoni, kampuni iliyokuwa ikimsimamia ilijitokeza katika mahojiano ya simu na Radio Jambo na kueleza sababu za kuvunja mkataba wao naye.

“Kufuatia tuhuma zisizo sahihi na zisizo halali, na uongo mwingi ambao umetolewa ambao umeharibu sifa ya kampuni, ndiyo maana timu nzima imekaa na kutoa uamuzi kwamba tutoke nje ya mkataba. ,” mwakilishi wa MIB alisema.

Kampuni hiyo pia likanusha madai kudhibiti na kuendesha akaunti za Stevo Simple Boy za mitandao ya kijamii na za kifedha.

“Unaeza endesha aje akaunti ya benki inayomilikiwa na mtu mwingine? Benki hutumia alama za vidole nitatumia aje akaunti yake ya benki ilhali sina alama zake za vidole? Ako na akaunti zake na yeye mwenyewe anazimiliki na kuziendesha. “