Babangu alikufa bila kuongea kwa matanga ya chifu - Gaucho

Gaucho alimshukuru Raila kwa kumpa jukwaa la kuzungumza kwa watu wengi wenye hadhi kubwa kama Uhuru Kenyatta, jambo ambalo marehemu babake hakufanikiwa kulifanya enzi za uhai wake.

Muhtasari

• "Ningeendaje kwa Uhuru bila kupata ridhaa ya Baba, ingekuwa ni kama kumkosea heshima, kama niko na kiherehere,” - Gaucho.

• Mwanaharakati huyo alisema kuwa baadae kuliibuka vita vikali dhidi yake na watu ambao wamo ndani ya Azimio.

Gaucho amshukuru Odinga kwa kumpa jukwaa la kukutana na Uhuru.
Gaucho amshukuru Odinga kwa kumpa jukwaa la kukutana na Uhuru.
Image: Facebook

Rais wa bunge la wananchi Calvince Gaucho amefichua kwa nini alitaka kwanza kumuomba Raila Odinga ruhusa kabla ya kukubali mwaliko wa kukutana na Uhuru Kenyatta mwezi mmoja uliopita.

Katika mahojiano na Oga Obinna, Gaucho alisema kwamba Uhuru Kenyatta mwenyewe alimuahidi kuutana naye na kumpa kile alichotaja kama ‘chai’ baada ya kumtambua kwa ukakamavu wake wa kukipigania chama cha Jubilee ambacho kiko katika mtihani mgumu huku kukiwa na mgawanyiko mkubwa baina ya wanachama wake.

Gaucho alisema kuwa alikubali mwaliko huo lakini alitaka kwanza kupata tamko la Odinga kabla ya kuutana na Kenyatta katika kile alisema kuwa Odinga ndiye amekuwa nguzo kubwa sana kwake kumfanya kujuana na hata kupata nafasi ya kuzungumza mbele ya viongozi wakubwa kama rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Gaucho alisema kuwa kama si familia ya Odinga, yeye asingejulikana na mtu yeyote, huku aksiema kuwa angalau kupitia kwa Odinga amepata kusimama na kuzungumza mbele ya watu wenye hadhi ya juu, jambo ambalo babake hadi kufa kwake hakuweza kufanikiwa kulifanya.

“Nilimwambia lazima niongee na Baba kabla nikuje. Unajua hakuna sik ushingo itapita kichwa. Unajua Baba yako ni baba yako, huwezi piga boma bila yeye kukupa Baraka. Kama si yeye – familia ya Raila Odinga, ningeongea kwa jukwaa kubwa kama lile, kama baba yangu alikufa bila kuongea kwa matanga ya chifu, ama kwa mzee wa kijiji. Sasa ningeendaje kwa Uhuru bila kupata ridhaa ya Baba, ingekuwa ni kama kumkosea heshima, kama niko na kiherehere,” Gaucho alieleza.

Mwanaharakati huyo alisema kuwa baadae kuliibuka vita vikali dhidi yake na watu ambao wamo ndani ya Azimio.

Alisema kuwa vita hiyo ilichangiwa na tamko la Uhuru kutaka kumpa chai.

“Hata hii vita yote ambayo imekuwa sijui nini nini, najua imechangiwa na hiyo stori ya Uhuru kusema ya kwamba anataka kumpea Gaucho chai. Kwa hiyo napakwa matope. Hao watu wanajaribu vile nitafanya nini…” alisema.