Mamake muigizaji mkongwe mwanzilishi wa filamu za Bongo, Steven Kanumba, Bi Flora Mutegoa amesema kuwa kuna tukio ambalo lilitokea wakati wa msiba wa mwanawe na kilimuuma sana na ndio maana hapendi kukizungumzia.
Katika mahojiano na Global TV Online, alisema kuwa hatokaa kusahau jinsi alivyofukuzwa kwenye nyumba ya kupanga katika msiba wa mwanawe.
Mama mtu alisema kuwa katika maisha yake ya miaka Zaidi ya 60, amepitia changamoto nyingi lakini ile moja ambayo hawezi kuisahau ni kufukuzwa katika nyumba alikokuwa akiishi wakati wa msiba wa mwanawe.
“Changamoto ni nyingi sana kwa mfano nilipata changamoto moja kubwa, sipendi kuiongelea lakini iliniumiza kimaisha. Mimi nilifukuzwa kwenye nyumba nikiwa kwenye msiba wa mwanangu lakini nilimwambia Mungu ahsante, nikawaza mwanangu angekuwepo hili tatizo lingeisha,” alisema Bi Mutegoa.
“Walionifukuza ni watoto wa marehemu ndugu zangu niliokuwa nawalea. Waliniambia shangazi toka. Tupe nyumba yetu!” alikumbuka mamake Kanumba.
Hii si mara ya kwanza kwa mkongwe huyo kudai kwamba alianza kuona maisha kuwa shubiri baada ya kifo cha mwanawe.
Katika mahojiano mengine miezi kadhaa iliyopita, Bi Mutegoa alisema kuwa alizuiliwa kabisa kutumia picha za mwanawe baada ya kifo chake, akisema kuwa hakuwa na hatimiliki kwa sababu mwanawe alikuwa anajitoa katika kila kitu kwa kuwafurahisha watu.
“Kwa bahati mbaya, wakati Kanumba anafanya kazi zake, alikuwa anauza kila kitu, mpaka yaani na roho yake. Kwa hiyo mimi sina haki yoyote ya ile kazi ya Kanumba. Wanaofaidika ni wale. Na kwa bahati mbaya wengine hata hofu ya Mungu hawana, kuna mmoja nilimuomba kutumia picha za Kanumba kwenye filamu ya kumbukumbu za Kanumba, hakuwa tayari kunipa ushirikiano,” Bi Mutegoa, mamake na marehemu Kanumba alisema kwa mfadhaiko mkubwa.