Kwa mara nyingine mamake Kanumba, Flora Mutegoa amesimulia jinsi kifo cha ghafla cha mwanawe kinavyoendelea kumuua, Zaidi ya miaka 10 tangu kufariki.
Bi Mutegoa alisema kwamba kitu kikubwa amejifunza kutoka kwa maisha tangu mshangao ule wa mwaka 2012 baada ya Kanumba kufa ni kwamba duniani watu wengi watakuvunja moyo lakini tiba kamili ni kusamehe na kuacha mengine yapite.
Katika mtindo huo huo, Bi Mutegoa alitamka kwa mara nyingine kwamba alipata maisha mapya baada ya kuwasamehe wote waliotaka kumuumiza iwe kwa kupenda au kwa kutotaka, lakini akasisitiza kwamba kifo cha mwanawe katu hakikuwa mapenzi ya Mungu kama ambavyo wengi wanamfariji.
Mama huyo ambaye alisema ana umri wa miaka Zaidi ya 60 licha ya kuonekana bado mdogo alisema kuwa siri ni kusamehe lakini pia kuutoa moyo wako kwa Mungu.
“Siri ya mimi kuonekana hivi jinsi nilivyo, kwanza Moyo wako ukiukabidhi kwa Mungu unatulia. Unasamehe yote yaliyopita, unaanza upya. Na unamuachia Mungu. Huzeeki. Kwa Mungu hakuna mzee,” alisema.
“Ni mengi mno nimesamehe kwa mfano kama kifo cha mwanangu Steven Charles Kanumba, nimesamehe. Hicho ndio kikubwa. Unajua mengine ni mipango ya binadamu. Mtu akiumwa, utamwangalia, utampa Panadol lakini kile kifo cha kuuawa ni mapenzi ya binadamu na mimi ndani ya Moyo wangu nilisamehe na nimesamehe,” alisema.
Mama huyo pia alisema kuwa ndani ya nyumba yake, asilimia kubwa ya mapambo kwenye kuta ni picha za mwanawe, jambo ambalo linawafanya wengi kuamini kuwa Kanumba ndio alikuwa mtoto wake wa pekee kumbe sivyo.
Alisema Kanumba alikuwa mtoto wake kitinda mimba na ndio mvulana pekee, akisema kuwa wakubwa zake ni wasichana na wako.
Alipoulizwa iwapo nduguze Kanumba hawana shinda na picha za marehemu Kanumba kuwepo kwenye kuta hali ya kuwa zao hazipo, alisema kuwa hawana tatizo kabisa na hilo, lakini pia akasema kuwa siku hizi enzi ya kidijitali wengi huwa na picha kwenye simu zao na wanasahau kuzichaisha na pengine kuzitundika kwenye kuta.