Binti wa rais Charlene Ruto alia kushambuliwa na nyuki

“Siku ya Jumatano niliumwa mara tatu na nyuki, Uzuri sikufura sana😅" - Charlene Ruto alisema.

Muhtasari

• “Kati ya Jumanne na Jumatano nilitembelea mizinga ya nyuki ya babu yangu ili kusaidia kusafisha na kuvuna asali yao" - Charlene.

Charlene Ruto afichua sababu ya kuita mzinga Bottom Up.
Charlene Ruto afichua sababu ya kuita mzinga Bottom Up.
Image: Twitter

Binti wa kwanza wa taifa, Charlene Ruto ambaye ni mkulima hodari wa nyuki amelia kwamba mapema wiki jana alipotembelea shamba la nyuki la babu yake alishambuliwa na nyuki na kumuuma mara tatu.

Charlene alipakia rundo la picha na video kwenye Twitter yake akitoa maelezo mafupi kwa kila picha na video ambapo alisema kuwa nyuki walimuuma mara tatu baada ya zipu ya wanda lake la kujikinga dhidi ya mishale ya nyuki kukataa kufungika yote.

“Kati ya Jumanne na Jumatano nilitembelea mizinga ya nyuki ya babu yangu ili kusaidia kusafisha na kuvuna asali yao. Walikuwa na asali nzuri. Siku ya Jumatano niliumwa mara tatu kwa sababu zipu ya suti yangu haikufika mwisho (hatuwezi kamwe kuzungumzia usalama na tahadhari zinazohitajika katika ufugaji nyuki),” Charlene alisema.

Hata hivyo baada ya kuumwa na nyuki, binti wa kwanza wa taifa alijitapa akisema kwamba hakupata uvimbe unaosababishwa na mishale mikali ya nyuki, huku akisema kuwa shughuli ziliendelea kama kawaida.

“Uzuri sikufura sana😅 Hatukuvuna asali hii kwa sababu bar hiyo inatoka kwenye Brood box... imekaguliwa na kurudishwa...iko na nyuki wanaokuja,” Binti Ruto alisema.

Binti huyo wa kwanza amekuwa akijitahidi sana katika ukulima wa kufuga nyuki ambapo mwezi Aprili alilazimika kuhadithia jinsi alivyoafikia uamuzi wa kuita mzinga mmoja kwa jina la Bottom Up, kauli mbiu ambayo inahusishwa na sera za kisiasa za babake, rais Ruto.

“Tulipokuwa tukifanya ukaguzi kwenye mizinga, tuligundua kuwa baadhi ya nyuki walikuwa wamevamia mzinga ambao ulikuwa umetegwa kichwa chini na kuanza kutengeneza masega ya asali. Tuligeuza mzinga kuwa wima, tukavuna asali iliyopo na kuupa jina la "Bottom Up" kwa uchunguzi rahisi wa maendeleo yake,” Charlene alifafanua.