logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Stevo Simple Boy aangukia dili la kutumia wimbo wa 'Mihadarati' kuelimisha vijana

"Pia nimepigia simu NACADA na tayari tumeanzisha mazungumzo ya kukutana nao" - Mutua.

image
na Davis Ojiambo

Burudani06 July 2023 - 11:11

Muhtasari


  • • Kwa upande wake, Stevo alisema kuwa kufanya kazi na NACADA ni ndoto yake ya muda mrefu na hiyo nafasi ikija kujipa atakuwa ni wa kushukuru sana.
Mutua kumuunganisha Stevo na NACADA.

Baada ya wiki moja kupita tangu mkurugenzi mkuu wa MCSK Dkt Ezekiel Mutua kuahidi kumpa msanii mwenye matatizo makubwa Stevo Simple Boy kazi, hatimaye wawili hao wamekutana na Mutua kutimiza ahadi yake.

Mutua alimualika Stevo kwenye ofisi zake Jumatano na katika mazungumzo na vyombo vya habari za mitandaoni, Mutua alifichua kwamba jambo la kwanza alimlipia Stevo ada ya kujiunga kuwa mwanachama wa MCSK baada ya kugundua kwamba hakuwa mwanachama.

Mutua pia alifichua kwamba tayari ameshamteua Stevo kama balozi wa masuala ya vijana kwenye MCSK ingawa pia Stevo nia yake ni kuwa balozi wa kutoa tahadhari dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya – ambalo ni tatizo kubwa kwa vijana wengi nchini.

“Tumekubaliana kwamba tutafuata mwongozo ambao tulielewana kuwa atakuwa balozi wa vijana MCSK ili kuendeleza masuala ya muziki, kutuwakilisha katika mambo ya muziki, kuhimiza vijana. Pia nimepigia simu NACADA na tayari tumeanzisha mazungumzo ya kukutana nao kwa sababu anataka kuwa balozi wa kampeni za kuhubiri madhara ya matumizi ya dawa za kulevya,” Mutua alisema.

Alisema kuwa katika mkondo huo wa kupigana dhidi ya dawa za kulevya, Stevo atafaa pakubwa kwa wimbo wake wa kwanza ‘Mihadarati’ – jambo ambalo alilitaja kama tatizo la kitaifa ambalo limevaliwa njuga na rais na naibu wake nchini.

“Ingekuwa vizuri kama NACADA wangeungana, lakini sisi kama MCSK tutakuwa mstari wa mbele kumtumia kama kuna matamasha ambayo anaweza kutuwakilisha,” Mutua alimwambia msanii huyo.

Kwa upande wake, Stevo alisema kuwa kufanya kazi na NACADA ni ndoto yake ya muda mrefu na hiyo nafasi ikija kujipa atakuwa ni wa kushukuru sana.

“Kufanya kazi na NACADA nilikuwa na ndoto tangu kitambo. Wakati nilitoa hiyo ngoma ya Mihadarati Mungu alisema wewe utafanya kazi na NACADA, kwa hiyo, hatimaye Mungu ametenda. Wacha tuombe kila kitu kiende vizuri, tufanye kazi ya kuelimisha vijana,” Stevo alisema akishukuru Mutua kwa kumshika mkono.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved