Mwanamuziki wa Tanzania, Sharif Said Juma almaarufu Jay Melody amekamatwa na polisi nchini Kenya kwa madai ya kumshambulia promota mmoja jijini Mombasa anayefahamika kwa jina Golden Boy.
Kutokana na tukio hilo polisi mjini Nairobi walimkamata na kumpeleka katika kituo cha polisi cha Kilimani ambapo anasubiri kufunguliwa mashtaka.
Katika Video zilizochapishwa na chaneli ya YouTube, Plug TV, wasanii pamoja na watu wengine maarufu kama Jaguar, Brown Mauzo na meneja wake pamoja na wakili wake walifika katika kituo cha polisi kumjulia hali.
Promota Golden Boy akizungumza mitandaoni alisema kuwa ugomvi baina yake ulitokea baada ya watu waliokuwa na msanii Jay Melody kumshambulia.
“Kulikuwa na kutoelewana kidogo na nikavamiwa na nilihisi kwamba halikuwa jambo sahihi kwangu kufanyika. Kweli nilipigwa na Jay na watu waliokuwa naye.”
Aidha baada ya Jaguar kuingililia kati mwanamuziki huyo wa Bongo Fleva aliachiliwa huru.
Jaguar alimteteta Jay Melody akisema kuwa haikuwa shambulizi kutoka kwa mwanamuziki huyo mwenyewe bali ni meneja wake aliyehusika.
“Meneja wa Jay Melody’s na promota anayeitwa Golden walikuwa na mvutano siku ya Jumamosi katika tamasha moja la Jay. Kwa hivyo Golden alishtaki tukio hilo na ndiyo sababu tuko hapa. Lakini Sonko na mimi tumeingililia kati na tumewaleta pamoja na swala zima sasa limetatuliwa.” Jaguar alisema.
Hii si mara ya kwanza mwanamuziki kutoka taifa jirani ya Tanzania amehusika katika rabsha na kujipata katika njia panda na polisi wa hapa nchini. Mwaka jana, Harmonize alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Kilimani kwa madai ya kukosa kuhudhuria tamasha alilopaswa kutumbuiza licha ya kupokea malipo.