Staa wa Dancehall wa Jamaica, Tommy Lee Sparta kutumbuiza nchini Kenya

Mwimbaji huyo wa Dancehall atazuru Kenya, Gambia na Ghana kati ya Oktoba 26 na Novemba 30.

Muhtasari

•Taarifa hiyo ilifichua kuwa ziara ya Tommy Lee barani Afrika itakuja baada ya kutumbuiza katika nchi saba barani Ulaya.

•"Ziara hii itakuwa sherehe ya muziki, utamaduni, na umoja ambao hungependa kukosa!" Tommy Lee alitangaza.

Image: FACEBOOK// TOMMY KEE SPARTA

Staa wa Dancehall wa Jamaica Leroy Russell Junior almaarufu Tommy Lee Sparta amefichua mpango wake wa kutumbuiza nchini Kenya baadaye mwaka huu.

Katika taarifa yake siku ya Ijumaa, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 35 alitangaza kuwa atazuru nchi tatu za Afrika ambazo ni Kenya, Gambia na Ghana kati ya Oktoba 26 na Novemba 30 katika ziara iliyopewa jina la 'The Freedom Tour.

Taarifa hiyo ilifichua kuwa ziara ya Tommy Lee barani Afrika itakuja baada ya kutumbuiza katika nchi saba barani Ulaya.

"Habari kila mtu, ni Tommy Lee Sparta hapa na nina tangazo maalum kwa mashabiki wangu wote wa ajabu huko nje! Ninafuraha kuwafahamisha kwamba Roots Vibes Promotion inaleta nguvu yangu ya kusisimua na shoo za kuvutia Ulaya na Afrika kwa ziara ya kustaajabisha!

Kuanzia tarehe 26 Oktoba hadi 30 Novemba, nitakuwa nakanyaga jukwaa katika nchi mbalimbali za Ulaya zikiwemo Hispania, Ubelgiji, Uholanzi, Ujerumani, Sweden, Ufaransa na Denmark! Jitayarisheni kushuhudia talanta yangu ya ajabu moja kwa moja tunapounda kumbukumbu zisizoweza kusahaulika pamoja," Tommy Lee alitangaza katika taarifa.

Aliongeza, “Lakini si hilo tu! Pia nina furaha kubwa kushiriki kuwa tutaelekea Afrika pia! Kenya, Gambia, Ghana, jiandaeni!!! Tutakuwa na burudani kamili pamoja!

Siwezi kungoja kuwaona nyote na kushiriki muda mzuri na kila mmoja wenu. Ziara hii itakuwa sherehe ya muziki, utamaduni, na umoja ambao hungependa kukosa!

Hakikisha umeweka alama kwenye kalenda zako na ukae karibu ili upate masasisho zaidi kuhusu mauzo ya tikiti na maeneo."

Mwanachama huyo wa zamani wa Kundi la Gaza lililoongozwa na Vybz Kartel pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru mashabiki wake kwa kuendelea kumsapoti na kuwahakikishia upendo na heshima yake kwao.

"Ninatazamia kutikisa jukwaa na kuunda kumbukumbu zisizoweza kusahaulika nanyi nyote. Tuifanye ziara hii kuwa ya hadithi!,” Alisema.

Tommy Lee alipata umaarufu takriban mwongo mmoja uliopita baada ya kuchukua tasnia ya Muziki wa Dancehall kwa msisimko na nyimbo kadhaa maarufu zikiwemo Psycho, Shook miongoni mwa zingine. Ni miongoni mwa wasanii wanaotambulika zaidi wa Dancehall kutoka Jamaica humu nchini Kenya.