Jose Chameleone alibaki kinywa wazi alipoitisha teksi, ikaja yenyewe bila dereva - video

Msanii huyo alipigwa na butwaa baada ya kuona jinsi teksi hiyo ya robot ilivyokuwa inatii masharti ya barabarani ikiwemo taa za trafiki, kupita magari mengine, kuongeza na kupunguza kasi yenyewe.

Muhtasari

• Chameleone alipata uzoefu huu wa kipekee akiwa huko Phoenix.

• Wamarekani wengi wameanza kufanya majaribio ya magari yanayojiendesha yenyewe.

Chameleone ashangaa kuabiri teksi ya Robot
ROBOT: Chameleone ashangaa kuabiri teksi ya Robot
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji mkongwe wa lebo ya Leone Island Music Empire nchini Uganda, Jose Chameleone alibaki kinywa wazi baada ya kuitisha teksi kupitia programu ya mitandaoni ya usafiri na teksi hiyo ikaja na kumsafirisha bila kuendeshwa na dereva.

Msani huyo kupitia Instagram yake alipakia video hiyo ikimuonesha ameketi katika kiti cha abiria nyuma ya anapokaa dereva na gari hilo la Waymo Driver lilionekana kujiendesha lenyewe bila dereva.

Kilichoonekana ni usukani ukijizungusha wenyewe na kutia breki kila lilipofika kwenye taa za trafiki.

Kwa mujibu wa maelezo kwenye tovuti ya kampuni hiyo ya usafirishaji wa teksi, Waymo LLC, ambayo zamani ilijulikana kama Mradi wa Magari ya Kujiendesha ya Google, ni kampuni ya Kimarekani ya teknolojia ya kuendesha gari inayojiendesha yenye makao yake makuu huko Mountain View, California.

Waymo kwa sasa wanaendesha huduma za teksi za kujiendesha kibiashara huko Phoenix, Arizona na San Francisco, CA

Chameleone alipata uzoefu huu wa kipekee akiwa huko Phoenix.

Kiendeshaji cha Waymo ni kielelezo cha teknolojia inayojiendesha kikamilifu ambayo hudumisha udhibiti wa njia nzima kutoka kwa kuchukua hadi kuacha.

Magari yanayojiendesha ya Waymo hayahitaji hata abiria wao kujua jinsi ya kuendesha. Dereva wa Waymo atawasafirisha kwa usalama hadi wanakoenda, na kuwaruhusu kuketi, kupumzika na kufurahia safari.

Wamarekani wengi wameanza kufanya majaribio ya magari yanayojiendesha yenyewe.

Akishangazwa na teknolojia katika gari hilo, Chameleone aliona upandaji wake kwenye gari kuwa wa kushangaza kabla ya kuhoji teknolojia inaelekea wapi.

“Teknolojia ya ajabu    taxi bila dereva 😳 #Robotic 🚙 #Taxi #Waymo Tunaelekea wapi pia??”

Mwimbaji huyo alishiriki kipande cha video kupitia mitandao yake ya kijamii akiwa ameketi kwenye kiti cha nyuma cha dereva wa Waymo, huku akionekana kufurahia safari ya kuelekea kusikojulikana.

Hii hapa video;