Muda mchache baada ya video ya mwimbaji wa injili Justina Syokau kuibuka mitandaoni akimlilia kwa uchungu mchungaji wa kanisa la New Life Church huko Mavueni kaunti ya Kilifi, Ezekiel Odero kwa msamaha, mchungaji huyo amemjibu kwa njia ya kiungwana.
Syokau alikiri kuwa alimkosea Ezekiel kipindi alikuwa anahangaishwa na polisi kwa kuhusishwa na sakata la mauaji ya Shakahola.
Katika video hiyo, alisema kwamba baada ya mchungaji huyo kuwekwa chini ya ulinzi na polisi, alifanya video akionesha kufurahia kwake kwa madai kwamba Ezekiel aliwahi fanya mahubiri akiwakemea kina mama wanaowalea watoto bila baba zao kuwa hawana nyota ya ndoa.
Kwa machozi, alikiri kuwa tamko hilo limekuwa likimuuma sana kwani tangu hapo alipoteza nyota ya kazi na hajawahi kuitwa katika matamasha kutumbuiza, huku pia akiongeza kuwa mwanawe ni mgonjwa sana.
Ezekiel katika video iliyoibuka kwenye mtandao wa TikTok pia, alimjibu Syokau akisema kuwa hana ubaya na yeye na ameshamsamehe kitambo hata kabla yake kuwazia kuomba radhi.
“Jana niliona kwenye TikTok dada mmoja aliyekuwa mwimbaji nadhani bado ni mwimbaji, niliposhikwa aliongea maneno mabaya juu yangu. Mimi sikujua na huwa sishughuliki. Tena baadae alirudi akitubu kwamba pasta niliongea vibaya kukuhusu nisamehe mtumishi wa Mungu. Namuomba Mungu wangu amsamehe na abarikiwe. Sababu hakujua kile alichokuwa anasema,” Odero alisema.
Mchungaji huyo aliwatia changamoto waumini wake akisema kuwa kama kweli mtu una upendo wa kweli unahitaji kumsamehe na kumpenda yule ambaye anakuonesha chuki.
“Kama kweli una upendo wa dhati, basi unastahili kuwaonesha wabaya wako upendo, unawapenda hata wale wanaokuchukia,” aliongeza.