Msanii wa injili Justina Syokau hatimaye amekiri kwamba yeye ni mchekeshaji tu ambaye anafanya sarakasi ili kuwafurahisha Wakeya.
Katika video ambayo alifanya na kupakia TikTok yake akilia kwa kuwaomba wote aliowakosea msamaha, Syokau alisema kwamba Wakenya wanaomsuta kwa vitimbi vyake wanafaa kujua kwamba yeye ni mchekeshaji tu na si vinginevyo.
Syokau aliwataka wanaomshuku kuhusu ucheshi kumuuliza mchekeshaji wa muda mrefu Churchill ambaye ndiye alimpa umaarufu mwishoni mwa mwaka 2019 wakati aliimba wimbo wa kukaribisha mwaka mpya wa 2020.
“Watu naomba mtu mnielewe mimi ni mchekeshaji tu. Hata wakati nilihit 2020 mkiuliza Churchill kabisa, tulipiga sho na ilikuwa so comical na nimekuwa nikiimba nyimbo za comedy, ni uchekeshaji tu tafadhali wale hamnielewi naomba muelewe kwamba kuna muda wa kila kitu. Kuna wakati naomba nyimbo za kanisani na wakati mwingine naimba nyimbo za kutafuta biashara,” Syokau alisema.
Msanii huyo pia alisema kwamba wakati aligonga vichwa vya habari kuhusu kubandika makalio feki, ulikuwa tu utani na kuwataka waliokerwa na kitendo kile kumsamehe akisisitiza kwamba alikuwa anawapa mashabiki wake kitu cha kuwatia tabasamu kwenye nyuso zao.
“Nilikuwa nataka tu watu kujua kwamba niko na mshepu. Si kwa ubaya, mimi hiyo ilikuwa tu comedy. Ni kitu tu cha kufurahisha watu, hayo maneno yote hayakuwa ya ukweli, nilikuwa nimeweka tu mkate na nilifanya kuwafurahisha ili mpate kitu cha kuzungumzia muache kuboeka juu kuna shinda nyingi huku Kenya watu tu wanataka kufurahi,” Justina alisema kwa kilio.
Msanii huyo alisema kwamba watu wengi wamekuwa wakimtupia maneno yasiyoweza kuchapishika kwa kusema kwamba anajificha nyumba ya injili kufanya matukio ambayo hayakubaliki na sehemu ya watu wanaoamini katika Biblia.
“Nikishindwa kutingisha makalio tutakulaje mimi na mwanangu, nitamsomesha aje? Naomba tu. Mimi nimeishiwa kwa sababu ya watu wanaongea vibaya kunihusu. Naomba tu Wakenya kwanza mnielewe kwamba mimi ni mtu tu mzuri,” alilia.