Mchekeshaji Eric Omondi amefichua kwamba mwanawe atazaliwa katika kipindi cha wiki chache zijazo lakini akasema kuwa ili mtu kuona sura yake, kuna masharti mengi ambayo mtu atahitaji kuafikiana nayo.
Omondi ambaye wiki moja iliyopita alifanya tafrija ya kuweka wazi jinsi ya mwanawe – binti – alisema kwamba mtu atahitaji kumlipa shilingi milioni 50 taslimu za kenya ili kuoneshwa sura ya mwanawe.
“Kuona sura ya mtoto wangu itakuwa pesa nyingi sana. Ili mimi kuweka wazi sura ya mtoto wangu, nitahitaji kupewa shilingi milioni 50. Yeyote atakayenipa pesa hizo hata kama ni gazeti mtaionea hapo. Sura ya mtoto wangu ni ngumu sana kuonekana,” alisema.
Akiulizwa mbona shilingi milioni 50, Omondi alisema haya;
“Nimeona tufanye bei rahisi kutokana na ugumu wa kiuchumi. Tukiweka bei ya kawaida haitokuwa vizuri, tumeweka bei ya chini kabisa. Kama uko hapo nje wewe ni gazeti sijui nini, nitakuuzia sura ya mtoto, wewe uoneshane vile unataka.”
Msanii huyo alisema kuwa hiyo si njia ya kuwalaghai watu kwani ni chaguo tu asiyetaka kumuona mwanawe na asitoe, si jambo la kushrutishwa.
“Nalipisha hela hiyo kwa sababu ni mtoto spesheli. Msisahau ni wa Eric Omondi, na kkwa kigezo hicho tu, milioni 50 inahusu. Ni mrembo sana, mimi nishamuona jana kwa scan. Tayari pale anapigwa scan namuona tu anatabasamu.”
Matakwa haya mapya ya Omondi yanakuja kwa kukinzana na yale aliyoyatoa siku chache zilizopita kuhusu mwanawe.
Awali Omondi alisema kuwa mwanawe atakapozaliwa hivi atamfungulia akaunti ya mitandaoni ambapo atakuwa anapakia picha zake.
Alijitapa kwamba mwanawe atazaliwa hivi na akaunti zake mitandaoni zitakua kwa kasi na kuzipiku za wasanii kama KRG, Ringtone na hata Khaligraph.