Hakuna watakatifu, sisi wote ni wachafu mbele ya Mungu - Ringtone akiri

“Nataka niambie tu watu kwamba katika dunia hii hakuna mtakatifu, sisi wote ni wachafu mbele za Mungu. Na kama kuna anayejiita mtakatifu anafanya Mungu kuonekana muongo"

Muhtasari

• “Cassypool ndiye alikwenda akaniripoti kwa YouTube, bila heshima, bila upendo alisema eti nimeiba huo wimbo." - Ringtone.

ringtone
ringtone

Ikiwa ni wiki yenye heka heka nyingi za kashfa dhidi ya msanii wa injili Ringtone Apoko kuhusu kudaiwa kulaghai jumba la kifahari mtaani Karen, msanii huyo hatimaye amefunguka.

Katika mahojiano na Vincent Mboya, Ringtone amefunguka kwa kusema kwamba binadamu wengi hawatakiani mema huku akisema kwamba katika dunia hii hakuna aliye mtakatifu kwani sisi wote ni wachafu mbele ya Mungu.

“Nataka niambie tu watu kwamba katika dunia hii hakuna mtakatifu, sisi wote ni wachafu mbele za Mungu. Na kama kuna anayejiita mtakatifu anafanya Mungu kuonekana muongo. Mambo mengine sitaki kwenda sana, ya mahakamani yakwenda kule na ya duniani yatabaki duniani pia,” Ringtone alisema.

Ringtone vile vile alipata kuzungumzia kuangushwa kwa wimbo wake alioweka kwenye YouTube kabla ya purukushani na polisi na kusema kwamba Cassypool ndiye aliyeripoti wimbo huo kwa ouTube kusababisha kuondolewa na mamlaka ya jukwaa hilo.

“Cassypool ndiye alikwenda akaniripoti kwa YouTube, bila heshima, bila upendo alisema eti nimeiba huo wimbo. Nashukuru Mungu kwa sasa hivi nimejieleza na YouTube wamekubali wimbo utarudi. Cassypool mahali popote ulipo ujue maisha si ya chuki, tutakiane mema, wewe unanitakia mabaya. Cassypool ni baadhi ya wale watu ambao wanafurahi mimi nizame. Angependa mimi nipotee kabisa sijui kwa nini yaani. Angekuwa yeye ndiye anashikilia tap ya hewa ya kupumua angekuwa ameshanizimia… mimi bado ni mwanamuziki na wimbo wangu nafurahi unarudi YouTube,” alisema.

Msanii huyo alifunguka haya baada ya kuibuliwa kwa kashifa kadhaa dhidi yake kwamba nyumba anayodai ni yake katika mtaa wa kifahari wa Karen si yake bali ameghushi hati.

Msanii huyo wikendi iliyopita alikamatwa na polisi lakini baadhi ya watu walihisi ni vitimbi tu alikuwa anafanya kwa kuwalipa polisi na kuwataka wamkamate.