Tuacheni tu tucopy muziki, bora tuwape mashabiki vitu vikali - Rayvanny

Amapiano ni muziki wa Afrika, Afrobeat ni muziki wa Afrika na sisi ni Bongo Fleva – maanake ni flavor tofauti kwa kutumia bongo zetu. - Rayvanny.

Muhtasari

• Wiki kama mbili zilizopita, Alikiba alimsuta vikali mwenzake Diamond Platnumz kwa kuburuzwa mitandaoni kwamba alikuwa amecopy nyimbo za Nigeria.

Rayvanny
Rayvanny
Image: Screengrab

Mkurugenzi wa lebo ya Next Level Music, Rayvanny amekuwa msanii wa hivi punde kujitosa katika gumzo kuhusu wasanii wa Bongo Fleva kukosa ubunifu asili na badala yake kuiga na kuiba miziki ya wasanii wenzao.

Akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni katika tukio kubwa la mzalishaji wa muziki S2Kizzy, Rayvanny alisema kuwa hakuna muziki wa mtu ambao ni wa asili ila kinachofanyikana ni wasanii kuiga kutoka kwa wenzao.

Msanii huyo alisema kuwa kiuhalisia, katika melody moja kuna melody 100 ndani yake, huku akiwataka wanaowasuta wasanii wa Bongo Fleva kuwa wanaiba beat kuwapa likizo kwani hata hao wengine vile vile wnafanay kuchukua beat zao.

“Wanakwambia kwenye melody moja kuna melody zingine 100, na muziki ni ule ule, chord ni zile zile, sema tu type ya muziki. Kwa hiyo mwisho wa siku ukisema Amapiano ni muziki wa Afrika, Afrobeat ni muziki wa Afrika na sisi ni Bongo Fleva – maanake ni flavor tofauti kwa kutumia bongo zetu. Sisi watuache tu tucopy lakini vitu view vikali. Na wengine wanacopy tu kwetu. Mwisho wa siku kitu kizuri ni kizuri tu, Amapiano si muziki wa watu ni muziki wa Afrika na sisi ni Waafrika,” alisema.

Wiki kama mbili zilizopita, Alikiba alimsuta vikali mwenzake Diamond Platnumz kwa kuburuzwa mitandaoni kwamba alikuwa amecopy sehemu ya melody za wimbo wa Spyro aliomshirikisha Tiwa Savage, Who’s your guy.

Alikiba alimshauri Diamond kuumiza kichwa ili kuibuka na kitu asili kisicho na mwenyewe, akisema kuwa hulka ya kuchukua melody za wasanii wengine ni kama kuudhalilisha muziki wa Bongo Fleva ambao ameupambania kwa miongo miwili sasa.

Hata hivyo, Spyro alijitokeza kupitia Twitter na kuwakomesha waliokuwa wanamburuza Diamond, naye akisema kauli sawia na ya Rayvanny kwamba hakuna muziki wa mtu, na katu hakutatokea msanii wa kusimama peke yake pasi na kuhitaji msaada wa wasanii wenzake wakiwemo wa sasa na waliotangulia.