Nadia Mukami amtema msanii Latinoh mwaka mmoja baada ya kumsaini kwenye lebo yake

"Ni biashara ngumu ambayo ina siasa nyingi sana na watu huwa hawajui kwamba ile pesa yako kidogo ndio unajaribu kusapoti…” Nadia alisema.

Muhtasari

• Nadia alisema kwamba kuwasaini wasanii ni jambo gumu lakini akasisitiza kwamba yeye atasalia kwenye mstari wake wa kuendelea kuwapa sapoti wasanii chipukuzi.

Nadia Mukani na Latinoh.
Nadia Mukani na Latinoh.
Image: Instagram

Msanii ambaye pia ni bosi wa lebo ya muziki ya Sevens Creative, Nadia Mukami amefunguka ni kwa nini msanii wake Latinoh hajaonekana kufanikiwa ikiwa ni Zaidi ya mwaka mmoja tangu kumzindua Februari mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni, Nadia alisema kwamba msanii huyo alikumbwa na ukakasi Fulani ulionuia kumng’oa kwenye lebo hiyo katika kile alisema kuwa kulikuwa na siasa nyingi.

Mukami alifunguka kwamba hafikirii katika maisha yake kama atakuja kumsaini msanii mwingine, akisema kumsaini msanii ni kibarua kigumu sana.

“Kusaini wasanii ni ngumu sana, watu wanaona kwamba rekodi lebo ndio mbaya lakini naweza sema ni ngumu sana naweza nikasema sidhani kama nitakuja kusaini msanii mwingine tena. Ni biashara ngumu ambayo ina siasa nyingi sana na watu huwa hawajui kwamba ile pesa yako kidogo ndio unajaribu kusapoti…” Nadia alisema.

Msanii huyo mpenzi wa Arrow Bwoy alisema kwamba kwa sasa wanasubiria Latinoh aachilie video zake ambazo alikuwa amefanya chini ya lebo hiyo na ambazo hazijatoka kabla ya kumuachilia kwenda zake.

“Kunakuwa na siasa nyingi, mtu anapewa ushauri huku na kule na kwa sasa niseme ni gumzo kuhusu, tulifanya EP yake na ni muda tu yeye kuachilia video za muziki wake na sisi tutamuachilia aende,” Mukami aliongeza.

Nadia alisema kwamba kuwasaini wasanii ni jambo gumu lakini akasisitiza kwamba yeye atasalia kwenye mstari wake wa kuendelea kuwapa sapoti wasanii chipukuzi lakini si kwa kuwapa mkataba Sevens Creative.

“Msininukuu vibaya, si eti sitasapoti wasanii lakini nitawasapoti kwa njia tofauti, si kwa kuwasaini,” Mukami alisema.