EXCLUSIVE

Rapa Diana Wairimu afunguka kwa nini alichagua "Wanja Kihii" kama jina lake la usanii

“Mimi naitwa Diana Wairimu kutoka Nyeri lakini napenda kuitwa Wanja Kihii juu mimi napenda kupanda miti." - Rapa huyo chipukizi aliambia Radio Jambo.

Muhtasari

• Msanii huyo chipukizi alisema yeye hufanya kila kitu kutoka ucheshi, sanaa na hata tiktok.

• Alisema kwamba haoni ubaya wowote wa kutumia jina hilo ambalo kwa jamii ya Kikuyu huchukuliwa nje ya muktadha.

Wanja Kihii.
Wanja Kihii.
Image: Screengtab//YouTUbe

Wikendi iliyopita, msanii chipukizi wa muziki wa kufoka, Wanja Kihii alikuwa gumzo la mitaani baada ya kuachia wimbo wa utani akiwalenga wasanii wa humu nchini lakini pia wa nje ya nchi.

Si tu jinsi alivyoimba wimbo huo, bali pia jina lake vilikuwa ni baadhi ya mambo ambayo yalizua minong’ono mitandaoni na kuwafanya wengi kutaka kujua haswa ni kwa nini aliamua kuchagua jina hilo – ikizingatiwa kwamba katika Kikuyu, ni jina au neno ambalo aghalabu huchukuliwa nje ya muktadha kuwa lisilo la heshima katika jamii hiyo

Katika mahojiano ya kipekee kwa njia ya Simu na Moses Sagwe, mwandishi wa Radio Jambo, Mrembo huyo ambaye tulibaini jina lake halisi ni Diana Wairimu alifunguka sababu za kuchagua kutumia jina hilo licha ya kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu athari zake.

Wairimu ambaye aliachilia wimbo wa kuwasuta na kuwadhihaki wasanii kwa jina ‘Zebra’ alisema kwamba anajua maana ya jina “Kihii” lakini aliamua kulitumia kwa vile ni jina la upekee wa aina yake.

“Mimi naitwa Diana Wairimu kutoka Nyeri lakini napenda kuitwa Wanja Kihii juu mimi napenda kupanda miti. Ilmradi ni mimi, siwezi hisi kama kuna ubaya wa kutumia jina hilo popote. Wanja Kihii ni bora kuliko Diana Wairimu,” alisema.

Akizungumzia wimbo huo ambao ulimpa umaarufu wa ghafla baada ya watu wengi kuueneza mitandaoni, Wairimu alisema kwamba licha ya wengi kuujua kama ni wimbo wa kuwadhihaki wasanii, wimbo wenyewe unaitwa ‘Zebra’.

Hata hivyo, Wairimu alikiri kwamba yeye ni msanii wa kufanya kila kitu kutoka ucheshi, usanii wa kurap na kila kitu mradi tu ki kwenye mabano ya Sanaa.

“Ngoma inaitwa Zebra juu natema mistari kama zebra. Hiyo ngoma ukweli ni diss track. Mimi ni kila kitu, kutoka usanii, tiktoker, ucheshi. Lakini huu ndio wimbo wangu wa pili, wa kwanza ndio nilitoka unaitwa Wanja Kihii,” alisema na kukiri kwamba ngoma ya pili, Zebra, ndio imempa jina.

Wairimu alisema kwamba yeye hufanya shughuli zake Nyeri lakini pia Nairobi.