Rapa chipukizi Diana Wairimu almaarufu Wanja Kihii amefunguka sababu zake kuwakoromea wasanii wengi wanaofanya vizuri kutka humu nchini kuhusu muziki.
Kupitia mahojiano kwa njia ya simu na mwandishi wa Radio Jambo, Moses Sagwe, Wanja Kihii alisema kwamba kwa maoni yake anahisi wasanii wa humu nchini hawafanyi vizuri na kusema kwamba japo Wakenya na mashabiki wake wanamjua kwa ngoma zisizozidi mbili, lakini anafanya vizuri kuwaliko wasanii wengi.
Msanii huyo aliyetamba wikendi kwa wimbo wa kuwadhihaki wasanii wa Kenya na Tanzania alisema kwamba muziki wake aina ya rap unakubaliwa kuliko miziki ya wasanii kama vile Khaligraph Jones, Mejja, Bahati na wengine.
Wanja Kihii alisema kwamba kwa sasa anatafuta collabo za kimataifa tu, lakini pia hakuweza kufutilia mbali uwezekano wa kufanya collabo na wasanii wa humu nchini kama Ssaru ikitokea nafasi – kama ambavyo anasikika akiimba kweney mstari mmoja katika wimbo huo wake.
“Mimi kulingana na rap yangu naona imeweza kuliko yao. Nilikuja kuwaonesha vile muziki wa rap unafanywa juu rap yao bado haiku vile. Bado sijatafuta collabo za humu nchini kama kutoka kwa Khaligraph, lakini kwa sasa tuseme natafuta collabo za kimataifa,” Wanja Kihii alisema.
“Ssaru ako sawa hata Khaligraph Jones pia anaweza nitafuta tufanye collabo naye. Pia Mejja, wote wanitafute niwaoneshe njia. Niwaoneshe vile ngoma inafaa kufanywa. Tofauti yangu na wao ni kwamba rap yangu ni kali kuliko yao, hiyo ndio kitu kiko,” aliongeza.
Katika wimbo wake ambao uliwachukua Wakenya kwa Mshangao, Wanja Kihii aliwadhuhaki wasanii wengi wa humu nchini, bila kubagua jinsia akisema kwamba yeye ndio malkia mpya wa muziki wa rap wa kizazi kipya.
Hata hivyo, wengi walihisi msanii huyo alikuwa anafanya mzaha na utani kwa jinsi alikuwa anaimba kwa sauti yake iliyojaa lafudhi ya Kikuyu na pia utunzi hafifu ambao ulikaa kichekesho Zaidi ya ushari wa nyimbo.
Maoni yako ni gani kuhusu Wanja Kihii kujitolea kuwapa mafunzo marapa wa humu nchini?