Mjasiriamali Betty Kyallo amezindua biashara mpya ya manukato ya kupendeza kwa mashabiki wake mitandaoni.
Kupitia Instagram yake, Kyallo ambaye amezamia katika ujasiriamali baada ya kuonekana kuondoka kwenye tasnia ya uanabahari alitangaza kwamba biashara yake ya manukato ghali ndio mwanzo imeng’oa nanga na kuwataka watu kujitokeza na kununua, akiwahimiza kwamba ujasiri wako unaanza na aina ya manukato unayotumia.
Hata hivyo, kilichowashangaza wengi ni bei ya manukato hayo.
Kyallo hakusita kuambatanisha kila aina ya manukato na bei yake, na mashabiki wengine walibaki vinywa wazi kuona bei ambayo kwa wengi ilionekana kuwa ghali kwa kichupa kidogo tu cha manukato hayo.
Moja ya manukato ambayo Kyallo alisema kwamba ndio angependa mpenzi wake kutumia yanaitwa Voyager, ambayo bei yake ni shilingi elfu 6 pesa za Kenya.
“Hii hasa inaitwa Voyager. Inafurahisha sana na haisahauliki. Hakika ni aina ya manukato nataka mtu wangu atumie. Kubali umaridadi na mvuto wa manukato haya ya kuvutia. Hadithi yako huanza na kila harufu. Bei: Ksh 6,000,” Kyallo alisema.
Alizidi mbele kuelezea upekee wa manukato hayo ambayo aliyasifia kuwa ndio angependa mpenzi wake kutumia ili kupendeza na kuvutia Zaidi anapokuwa karibu naye.
“Kuhusu Voyager: Hii ni harufu nzuri ya Mbao kwa wanaume. Maelezo ya juu ni Bergamot, Pink Pilipili na Clary Sage; noti za kati ni Vetiver ya Haiti na Ngozi; maelezo ya msingi ni Ambroxan, Akigalawood, Indonesian Patchouli Leaf na Cacao Pod.”
Mrembo huyo mama wa mtoto mmoja ameendeleza kupiga hatua zake ikiwa ni pamoja na kuzindua matawi mbalimbali ya biashara yake ya saluni nchini.
Wengi walimjua Kyallo kama mwanahabari miaka michache iliyopita lakini baada ya kuondoka kwenye runinga, mrembo huyo alijikita Zaidi katika kujiendeleza kama mfanyibiashara haswa katika kitivo cha bidhaa na huduma za kurembesha muonekano wa mtu.