Kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kurefu cha utata unaozingira baba halisi wa mwanawe mjasiriamali Hamisa Mobetto, mrembo huyo amejibu swali kuhusu hilo.
Katika mahojiano ya kipekee na waandishi wa habari za mitandaoni, mmoja alimuuliza Hamisa kuhusu utata unaozingira baba wa mtoto huyo ambaye awali ilikuwa inajulikana kama ni wa msanii Diamond.
Mobetto aliweza kuzungumzia kwa undani ni kwa nini Diamond hajawahi kiri wazi kwamba mtoto huyo ni wake na wala kupakia picha yake kweney kurasa zake wakati ambapo anasherehekea siku yake ya kuzaliwa – ya hivi karibuni ikiwa ni mapema wiki hii.
“Kwanza kabisa nisingependa kumuongelea mtoto wangu kwa sababu ni mwanangu wa miaka 6 anakua na kuna vitu ataviona. Nafikiri kwa mtoto, hilo si jambo zuri kwa ukuaji wake wa afya ya akili au kitu chochote, na pia sidhani kama ina kitu chochote cha kujielezea, nadhani muda wa kujielezea ulishapita,” Hamisa alisema.
Mrembo huyo mama wa watoto wawili alisema kwamba kitendo cha Diamond kufumbia jicho siku ya kuzaliwa kwa mwanawe wala hakijawahi kumpa msongo wowote wa kimawazo, akisema kuwa yeye siku zote huenda na mipango ya Mungu tu.
“Mimi niko vizuri na niko sawa, mimi ni mtu ambaye huwa naenda kutokana na mipango ya mwenyezi Mungu. Kwa hiyo kitu chochote ambacho Mungu atakifanya kwa wakati huu ama kitatokea hakiwezi kikaniathiri kwa neno lolote lile kwa sababu maisha tunayoishi yamepangwa, ninaamini hivyo,” aliongeza.
Akizungumzia ukakasi katika kauli hiyo yake ya kuashiria kwamba baba wa mwanawe si baba bora, Hamisa alisema kuwa hajataja mtu lakini mhusika anajijua tu.
“Sidhani kama nimetaja mtu wakati ninaongea. Mimi niliongelea mwanangu kwa sababu huyo ndio chaguo langu la kwanza kwangu, wanangu huja mwanzo na nilimaanisha kwamba ninalea mwanamume wa baadae mtoto wako wa kike atakuwa salama naye,” alifafanua.
Kuhusu mwanawe kufananishwa na Billnass, Hamisa alisema;
"Hakuna kitu chochote kinachoniingia nikiona mwanangu anafananishwa na Billnass kwa sababu naamini chochote kinachoeleweka hakiihitaji maelezo. Nadhani mimi nilishaongea wakati uliopita, Nenga pia naye alishaongea wakati wake na hakuna kingine ambacho kimebaki kuongea."