Mwigizaji Kajala Masanja ametoa onyo kali kwa mwanamuziki Marioo kuhusu kuja kumuacha binti yake Paula Kajala.
Kajala alipakia kionjo cha video ya wimbo wa Marioo kwenye Instagram yake na kukiri kwamba tayari msanii huyo ameshapeleka barua ya posa kwa familia yake kwa ajili ya kupata ndio ya kumchumbia mwanao Paula.
Kajala hata hivyo alitoa onyo kwa msanii huyo na kumuambia kwamba ikija kutokea wamekosana na wakaachana, Marioo hafai kuanza kumchamba kama ambavyo Harmonize amekuwa akimchamba yeye na bintiye mitandaoni.
Kajala alivuka mipaka hata Zaidi na kumtishia Marioo kwamba iwapo atafanya hivyo, basi hatokuwa na budi bali kumroga tu.
“Hongera son bonge moja la video, kuhusu barua ya uchumba tumeipokea kwa mikono miwili subiria majibu na karibu masanja family🤪 (ila mwakani usije ukatuchamba na wewe nitakuroga)” Kajala alisema japo kwa utani.
Ikumbukwe Paula na Marioo wamekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa miezi michache sasa japo bado wengine wanahisi ni kiki kutokana na mazingira mazima jinsi walitambulisha uhusiano wao ambao awali ulionekana kama ni kutafuta ile waingereza wanaita Chemistry kwa ajili ya wimbo wa Marioo ambao Paula alicheza kama vixen wa video.
Wakati huo huo, Harmonize na Kajala wamezama kwenye mfululizo wa kuchambana mitandaoni, Harmonize akimvua Kajala nguo bayana kuhusu mambo mbali mbali.
Mambo yalianza pale Harmonize alipoachia bonge la ngoma ya Dear Ex akiituma moja kwa moja kwa mpenzi wa zamani Kajala huku akimtuhumu kwa matukio mengi tu.
Harmonize katika moja ya mstari wa wimbo alimtaja Kajala na bintiye kama matapeli ambao lengo lao kwake liikuwa ni kumfyonza mali yote hadi kumuacha hoi taabani, jambo ambalo anajipiga kifua akidai kwamba halikufua dafu na ndio maana walikwenda zao kwa machungu.