Khaligraph Jones amtaja Octopizzo kama model wa Instagram

“Mimi sina uhasama na yeye, sina huo muda ukiona nimefikisha umri wa miaka 33... mimi nikikutana na Octo namsalimia ‘niaje’ akitaka aitike akitaka asiitike mimi nishamsalimia,”

Muhtasari

• Hata hivyo, Khaligraph alimchimba mkwara Octopizzo akimlinganisha kama mwanasosholaiti wa Instagram ambaye anafanya vizuri kwa upande huo.

Khaligraph Jones na Octopizzo.
Khaligraph Jones na Octopizzo.
Image: Instagram

Kwa mara nyingine tena, rapa Khaligraph Jones amezungumzia kuhusu ‘uadui’ wa kimuziki baina yake na rapa mwingine Octopizzo.

Akizungumza na Obinna, Khaligraph alisema kwamba yeye hana tatizo wala chui dhidi ya Octopizzo ila Octopizzo ndiye kama hampendi tu na wala hawezi kumlaumu kwa kumchukia.

Alisema kwamba yeye kwa sasa amefikisha umri wa miaka 33 na hana muda wa kuhasimiana na Octopizzo akisema kuwa wakati wowote akimkuta analazimisha kusalimiana naye bila kujali kama ataitikia salamu au la.

“Huyo mvulana hajawahi nipenda, unajua kuna tu mtu unahisi kama huwezi mpenda na huwezi mlaumu, ulizaliwa tu hivyo. Niliona kwa mahojiano akisema kwamba hanipendi vile ninavaa. Mimi namuelewa kwa sababu mimi sihisi kama mimi nahisi hivyo kuhusu mtu mwingine yeyote, lakini namuelewa kwa sababu hata ningekuwa yeye singependa Khaligraph,” alisema.

“Mimi sina uhasama na yeye, sina huo muda ukiona nimefikisha umri wa miaka 33, sasa vitu tulianza huko nyuma mpaka sasa hivi ni wapi na wapi, mimi nikikutana na Octo namsalimia ‘niaje’ akitaka aitike akitaka asiitike mimi nishamsalimia,” Khaligraph aliongeza.

Hata hivyo, Khaligraph alimchimba mkwara Octopizzo akimlinganisha kama mwanasosholaiti wa Instagram ambaye anafanya vizuri kwa upande huo.

“Anafanya kazi nzuri, ana kurasa safi sana kwenye mitandao ya kijamii. Octo ni mwanamitindo mzuri sana, anapiga modelling fiti sana na namheshimu sana kwa kazi hiyo. Jamaa alikuja kutoka Kibera na namheshimu sana kwa sababu alikuja kutoka mazingira magumu sana lakini mambo ya nani anajua kurap kushinda mwingine hiyo tuache,” Khaligraph alisema.